VIONGOZI WA SERIKALI WAASWA KUTOINGILIA MAAMUZI YA MABARAZA YA ARDHI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 5 May 2021

VIONGOZI WA SERIKALI WAASWA KUTOINGILIA MAAMUZI YA MABARAZA YA ARDHI

Mjumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilayani Nkasi Emmanuel Kushoka akiapa mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili kushoto) pamoja na viongozi wengine wa Wilaya ya Nkasi. 


Mjumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilayani Nkasi Albertina Kitaani akiapa mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) pamoja na viongozi wengine wa Wilaya ya Nkasi. 

MKUU wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaasa viongozi wa serikali Pamoja na Viongozi wa kisiasa kutunza uhuru wa mahakama kwa kutoingilia mashauri ama maamuzi yanayoafikiwa na mabaraza ya ardhi na nyumba mkoani humo hata kama wananchi watawafuata na kuwataka waingilie maamuzi hayo.

Ameelekeza kuwa suala likisha amriwa na baraza la ardhi na nyumba atakayeshindwa akate rufaa na sio kwenda kwa Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, Mbunge, Diwani au Mwenyekiti wa serikali ya mtaa au Kijiji kulalamikia maamuzi ya baraza.


“Vyombo vya kisheria vina utaratibu wake, kama hukuridhika na maamuzi, yaliyotolewa na baraza hili la ardhi na nyumba basi ngazi inayofuata ni kukata rufaa, kwahiyo unashauriwa ukate rufaa, mwisho lakini si kwa umuhimu, nimshukuru sana mheshimiwa Waziri wa Ardhi na Nyumba Pamoja na Naibu wake kwa kukubali kuanzishwa kwa Baraza la Ardhi katika Wilaya ya Nkasi na hatimae kuteua wajumbe,” Alisema.


Mh. Wangabo aliyasema hayo katika hafla fupi ya uapisho wa wajumbe wanne wa baraza la ardhi na nyumba alilolizindua leo tarehe 5.5.2021 katika ofisi hiyo mpya ya baraza hilo mjini mdogo wa Namanyerea, Wilayani Nkasi mbapo viongozi wote wa serikali na wa kisiasa walihudhuria hafla hiyo.


Akitoa ufafanuzi wa malalamiko wanayokutana nayo kutoka kwa wananchi, Mkuu wa Wilaya hiyo Mh. Said Mtanda alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa na tabia ya kukimbilia kwa mkuu wa wilaya pindi wanapoona mwenendo wa kesi zao haupo upande wao na hivyo kuomba kusaidiwa.


“Tulipata mwananchi mmoja kutoka (kijiji) Isale, anakuja kulalamika kwamba kesi yake ipo baraza (la kata) lakini anahisi kama atapoteza matokeo huko katika baraza, kwahiyo badala ya kwenda kusikiliza kesi yake hukumu inatolewa, ameamua kukimbilia kwa mkuu wa wilaya anasema kuwa usalama wake upo hatarini, tunamuuliza mbona umetoka isale mpaka hapa bado usalama upo, lakini ameshindwa kutoka nyumbani kwake kwenda kwenye baraza,” Alisema.


Kwa upande wake mmoja wa wajumbe waliokula viapo katika hafla hiyo akiwakilisha wajumbe wenzie Bwana Emmanuel Kushoka alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kupigania kupatikana kwa baraza hilo na kuanzishwa kwake katika wilaya hiyo.


“Kwahiyo sisi kama wajumbe kama ulivyoelekeza ni kwamba sisi au kama kiapo chetu tulivyoapa ni kwamba tutakuwa waadilifu na wa kutenda haki bila ya kupendelea upande wowote, kwa nafasi hiy tunashukuru na tunaahidi kwamba tutatenda haki,” Alisisitiza.


Baraza hilo la Ardhi na Nyumba Wilayani Nkasi limelenga kupunguza mwendo wa walalamikaji kufika Sumbawanga kusikiliza kesi zao na kuongeza idadi ya mabaraza hayo katika Mkoa kuwa mawili huku moja likiwa Wilayani Sumbawanga, wajumbe wa kwanza waliokula viapo katika kuendesha baraza hilo wakiwa ni Emmanuel Kushoka, Reminisere Usiri, Mary Siame, na Albertina Kitaani. 

No comments:

Post a Comment