MIKOPO YA NMB MASTA BODA SASA YATUA RASMI KANDA YA KASKAZINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 26 May 2021

MIKOPO YA NMB MASTA BODA SASA YATUA RASMI KANDA YA KASKAZINI

Kutoka Kushoto: Mwendesha bodaboda wa Jijini Arusha Stella Nguma, Mkuu wa kitengo cha Biashara wa Benki ya NMB Alex Mgeni, Mwenyekiti wa chama cha pikipiki za miguu mitatu Twaha Mpera, Mwenyekiti wa chama cha pikipiki za miguu miwili Okero Costantine, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Allan Rushokana, Kaimu Mkaguzi Mkuu wa ndani Benki ya NMB Benedicto Baragomwa na Meneja Mwandamizi wa Bidhaa, Clara Mwichumu, wakizindua kampeni ya Miliki Chombo jijini Arusha inayowawezesha waendesha bodaboda na bajaji kupata mikopo nafuu. Hafla ya Uzinduzi huo ilifanyika leo jijini Arusha katika Ukumbi wa  Lush Garden.



Baadhi ya waendesha boda boda na bajaji wa jijini Arusha wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi Allan Rushokana na wafanyakazi wa Benki ya NMB baada ya kufanyika uzinduzi wa Mikopo ya NMB Masta Boda  leo.

KUTOKANA na changamoto ya madereva boda boda na pikipiki aina ya miguu mitatu kutomiliki vyombo vyao vya kazi, Benki ya NMB imekuja na njia ya kuwakomboa na hali ya utegemezi kwa kuwapatia mikopo nafuu ya umiliki wa vyombo hivyo.

Hakimu Saimon ni katibu wa bodaboda mkoa wa Arusha alisema anaishukuru taasisi hiyo kwani wamekuwa wanaendesha pikipiki za wengine kwa muda mrefu hali inayopelekea kuwa tegemezi katika umiliki wa vyombo hivyo kwa kuwarejeshea wamiliki wao fedha waliopangiwa.

"Kwa kufanya hivyo wamekuwa wakiingia mikataba ya kurejesha sh.10,000 kila siku ndani ya miezi 13 ilikuwa ni mateso lakini kupitia benki ha NMB kila mmoja wetu atanufaika na mkopo huu na kuweza kumiliki chombo chake na kujikwamua kiuchumi katika kujiletea maendeleo,"alisema Katibu huyo.

Alisema ni jambo la furaha kwao kutumia fursa ya mkopo huo katika kumiliki vyombo vyao kwani wao watatoa asilimia 20 na 80 wataongeza Benki ya NMB hivyo watafanya juhudi katika marejesho hawatakuwa na mchezo katika kutumia fursa hiyo.

Kaimu Afisa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto   Baragomwa alisema baada ya uzinduzi huo waendesha bodaboda na bajaji watapata fursa ya kupata pikipiki za miguu mitatu na miwili ikiwa zoezi hilo lilianzia Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na sasa Arusha ikiwa mkoa unaofuata ni Mbeya.

Baragomwa alisema benki hiyo imetenga Sh. bilioni 5 kwa kuanzia kwa mwaka huu ambapo zitawanufaisha waendesha bodaboda zaidi ya milioni mbili nchini.

"Kwa kuwa bodaboda wengi ni vijana na hawana dhamana, NMB imekuja na njia ya kuwakopesha kwa mikopo nafuu. Ni vyema wakatumia fursa hii ili kila mmoja amiliki chombo chake," alisema.

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Arusha, Kenani Kihongosi katika uzinduzi huo, Afisa Afya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Allan Rushokana alisema swala la kuwakopesha mikopo hiyo madereva hao itawasaidia kuwaletea maendeleo yao na kujikwamua kiuchumi.

"Lengo kubwa la taasisi ya fedha ya NMB ni kuwasaidia kujikwamua kiuchumi kwani suala la ajira nchini limekuwa changamoto lakini kujiajiri kuna nyanja pana hivyo wazingatie utaratibu wa kupata mikopo ili kila mmoja aweze kumiliki chombo chake na mpango huu ukatoe matokeo mazuri katika kuleta maendeleo  na kujikwamua kiuchumi," alisema Mwakilishi huyo.

No comments:

Post a Comment