BANDARI MTWARA WATAKIWA KUFANYAKAZI KIKAMILIFU - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 9 May 2021

BANDARI MTWARA WATAKIWA KUFANYAKAZI KIKAMILIFU

 

Meneja wa Mamlaka ya Bandari Mtwara Eng, Juma Kijavara (wa pili kushoto), akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara alipokagua upanuzi wa gati, flow meter na mizani katika bandari hiyo.


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara akisisitiza jambo kwa viongozi wa Mamlaka ya Bandari Mtwara mara baada ya kukagua upanuzi wa bandari hiyo (kulia), ni mkuu wa Wilaya ya Mtwara Danstan Kyobya.

Muonekano wa sehemu ya kuhifadhia mizigo katika bandari ya Mtwara mara baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa kushoto ni wafanyakazi wa bandari hiyo wakimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara upanuzi wa gati la bandari hiyo.

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara ameitaka Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kuhakikisha bandari ya Mtwara inafanyakazi kikamilifu ili kuongeza mapato na kukuza uchumi wa mikoa ya kusini.

Akizungumza mara baada ya kukagua upanuzi wa bandari hiyo Mhe. Waitara amesema uwekezaji uliofanywa na Serikali katika bandari hiyo ni mkubwa hivyo unatakiwa kuleta tija kwa kuhakikisha bandari inatumika kikamilifu kubeba mizigo ili kuzalisha faida na kupunguza mzigo mkubwa unaosafirishwa kupitia barabara.

“Mmesema bandari hii ina kina kirefu na cha asili sasa tafuteni masoko ili mizigo mingi inayosafirishwa kwa kutumia barabara ianze kutumia bandari hii na hivyo kulinda barabara”, amesisitiza Waitara.

Amemtaka Mkurugenzi mkuu wa TPA kuangalia uwezekano wa kuondoa tozo zinazowakwaza wasafirishaji ili kuwezesha wafanyabiashara wengi kutumia bandari ya Mtwara,

Amempongeza Meneja wa Bandari Mtwara Eng. Juma Kijavara kwa usimamizi mzuri katika mradi wa upanuzi wa bandari hiyo na kutoa wito kwa wafanyabiashara kutumia bandari hiyo ili kupunguza msongamano katika barabara ya Mtwara-Dar es salaam.

“Bandari ikitumika kikamilifu uzalishaji wa shughuli za viwanda, kilimo na biashara utakuwa na barabara zitadumu kwa muda mrefu kwani mizigo mingi itapitia kwenye maji”, amesema Naibu Waziri Waitara.

Naye Meneja wa Bandari hiyo Eng. Juma Kijavara amemhakikishia Naibu Waziri Waitara kuwa bandari ya Mtwara imetenga eneo la kutosha la kuhifadhi mizigo ya wasafirishaji hivyo katika siku za karibuni itaanza kupokea shehena nyingi za mizigo.


Aidha amebainisha kuwa ukosefu wa reli inayounganisha mikoa ya kusini,  ukosefu wa meli za mwambao wa bahari ya hindi, kudhorota kwa shughuli za uchimbaji wa gesi na ukosefu wa viwanda katika mkoa wa Mtwara na Lindi ni miongoni mwa changamoto zinazoathiri matumizi ya bandari ya Mtwara.

Zaidi ya shilingi bilioni 157 zimetumika katika kukarabati gati, flow meter , mizani  na miundombinu ya kupakia na kuhifadhi mizigo katika bandari hiyo.




Meneja wa Mamlaka ya Bandari Mtwara Eng, Juma Kijavara (wa pili kushoto), akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara alipokagua upanuzi wa gati, flow meter na mizani katika bandari hiyo. 



Meneja wa Mamlaka ya Bandari Mtwara Eng, Juma Kijavara (wa pili kushoto), akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara alipokagua upanuzi wa gati, flow meter na mizani katika bandari hiyo.


IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI MEI 8, 2021.

No comments:

Post a Comment