Mkuu wa Wilaya ya Mkalama (katikati kulia) Mhandisi Jackson Masaka na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Maji, Rosemary Rwebugisa ( katikati kushoto) wakifungua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Maji uliopo Kata ya Nduguti Wilayani humo jana kwenye maadhimisho ya wiki ya Maji.
Na Mwandishi Wetu, Singida
HALI ya upatikanaji wa Maji safi na salama katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia 76.8% kutoka 65.8% ya sasa baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini kuchimba na kukarabati visima katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Meneja wa wakala huo (RUWASA) Wilaya Mhandisi Antidius Muchunguzi alitoa taarifa hiyo jana kwenye maadhimisho ya wiki ya maji wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji uliopo Kata ya Nduguti ukiwa ni miongoni mwa miradi inayoendelea na iliyotekelezwa katika Vijiji mbalimbali wilayani humo.
Mhandisi Muchunguzi alisema kwa sasa hali ya upatikanaji wa Maji katika Wilaya hiyo ni 65.8% lakini baada ya kukamilika Miradi ya Vijiji vya Kinyangiri,Ibaga,Kinyambuli,Mpambala,Ikolo,Lyelembo,Nkungi,Ipuli na Malaja hali ya upatikanaji wa Maji utafikia 76.8%
"RUWASA Wilaya ya Mkalama inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali vijiji, mingine tunakarabati na mingine tunachimba visima katika vijiji vya Nkungi,Ipuli na Malaja." alisema Muchunguzi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mara baada ya kuzindua mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jackson Masaka aliziagiza kamati za Maji na wananchi kwa ujumla kuitunza miradi hiyo ili iwe endelevu.
"Miradi hii ili iwe endelevu inahitaji usimamizi wa karibu.Wananchi mshiriki katika ulinzi wa miundombinu ya Miradi ya Maji na kushiriki kupanda Miti kwenye Vyanzo vya Maji." alisema Masaka.
Aidha ameagiza RUWASA na kamati za maji za vijiji kuhakikisha maji hayapotei huku fedha zinazotokana na ankara za maji akitaka zitumike katika kukarabati miundombinu.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Maji Rosemary Rwebugisa, aliwaagiza wananchi pamoja na kutunza miradi hiyo na vyanzo vyote vya maji ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji,kulipa Ankara kwa wakati ili huduma ziendelee kutolewa.
Rwebugisa alisema Wizara haitafikia malengo yake ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji na salama kama miundombinu ya miradi iliyotekelezwa haitatunzwa.
No comments:
Post a Comment