Makamu wa Rais mteule, Philip Isdor Mpango. |
RAIS wa Tanzania, Mh. Samia Hassan Suluhu leo amempendekeza aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Isdor Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania. Baada ya uteuzi huo Bunge lilimpigia kura kumuidhinisha kushika nafasi hiyo, ambapo kati ya wabunge 363 waliopiga kura wote walimkubali kwa asilimia 100.
Akitangaza matokeo hayo Bungeni mara baada ya uchaguzi kufanyika Spika Job Ndugai alisema kati ya wabunge 363 waliopiga kura wote walimpa kura za ndiyo, hivyo kupita kwa asilimia 100 ya kura zote. Mpango ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais Mteule, anatarajiwa kuapishwa kesho tarehe 31 Machi Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma na tayari Ikulu imetoa taarifa ya hafla ya kiapo cha kiongozi huyo.
Philip Mpango ambaye ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi, CCM, kwa mara ya kwanza aliteuliwa kuwa Mbunge kwa Uteuzi wa Rais John Magufuli kwa miaka 2015 – 2020, halafu baadaye aligombea Jimbo la Buhigwe Wilayani Kasulu na kuchaguliwa kwa miaka 2020-2025 kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Mpango alizaliwa tarehe 14 Julai 1957 katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma na kupata elimu ya msingi wilayani hapo kabla ya kuendelea na elimu ya Sekondari katika Seminari ya Itaga mkoani Tabora na baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya 1993–1996 akibobea kwenye masuala ya uchumi.
Kiongozi huyo mbobezi na mzoevu masuala ya uchumi amewahi kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kufanya kazi katika fani hiyo taasisi mbalimbali za Serikali na Benki ya Dunia kabla ya kurejea rasmi kwenye masuala ya siasa. Amekuwa waziri wa Fedha na Uchumi kwa zaidi ya miaka mitano hadi anateuliwa kushika nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment