NIMERIDHISHWA NA MAANDALIZI YA IBADA NA HESHIMA ZA MWISHO KWA JPM UWANJA WA UHURU- MAJALIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 20 March 2021

NIMERIDHISHWA NA MAANDALIZI YA IBADA NA HESHIMA ZA MWISHO KWA JPM UWANJA WA UHURU- MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam na mikoa jirani Machi 20 na kesho kutwa Machi 21, 2021 watapata fursa ya kushiriki Ibada ya kumwombea Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kutoa heshima za mwisho katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kukagua maandalizi ya tukio hilo Ijumaa, Machi 19, 2021, Mheshimiwa Majaliwa amesema ameridhishwa na maandalizi yanayofanywa chini ya usimamizi wa Kamati ya Kitaifa ya Maafa ambayo yeye mwenyewe ndiye Mwenyekiti wake akishirikiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla. 

Mheshimiwa Majaliwa amesema Ibada hiyo itatanguliwa na ibada nyingine itakayofanyika kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es salaam ambako marehemu amekuwa akiabudu wakati wote alioishi Dar es salaam.

Amesema wananchi wote wa Mkoa wa Dar es Salam na mikoa jirani wanaotamani  kumuaga aliyekuwa rais wao mpendwa ambaye amefanya mambo mengi na makubwa  jijini Dar es salaam na Tanzania kwa ujumla wafike uwanja wa Uhuru kuanzi saa 11 alfajiri amabapo watapokelewa na kuonyeshwa mahali pa kukaa.

Mheshimiwa Majaliwa amesema fursa ya kutoa heshima za mwisho itatolewa hadi saa 12 jioni na endapo itaonekana kuwa bado wapo watu wengi wanaotamani kutoa heshima za mwisho kwa mpendwa wao muda utaongezwa hadi  watakapomalizika.

Amesema Machi 22, 2021 mwili wa marehemu utasafirishwa kwenda Dodoma ambako maombolezo ya kitaifa yatafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri na waombolezaji wa mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani pamoja na wambolezaji kutoka nje ya nchi watapata fursa ya kushiriki na kutoa heashima za mwisho.

Machi 23, 2021 asubuhi mwili utasafirishwa kwa ndege kutoka Dodoma kwenda Mwanza ambako shughuli za maombolezo zitafanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba na wananchi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa jirani watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.

Mheshimiwa Majaliwa amesema, Machi 24 mwili wa marehemu utasafirishwa kwenda Chato ambako wananchi wa Mkoa wa Geita na mikoa jirani watapata fursa ya kumuaga marehemu. Amesema Machi 25 mapema asubuhi  itafanyika Ibada nyumbani kwa marehemu Chato ikifuatiwa na mazishi.

Awali, Mheshimiwa Majaliwa alikwenda Ikulu Ndogo jijini Dar es salam kutoa pole kwa Mjane wa Marehemu Mama Janet Magufuli pamoja na familia na baadae alikwenda kwenye Viwanja vya Karimjee kutia saini kitabu cha maombolezo.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kuwa anafarijika kuona kwamba siku zote umekuwepo ushirikiano wa dhati kati Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika nyakati za shinda na raha.

No comments:

Post a Comment