Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Abdallah Ulega akisisitiza jambo.
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Abdallah Ulega ameiagiza Idara ya Michezo ya Wizara hiyo, kukaa pamoja na Taasisi zinazosimamia sekta ya michezo nchini kujadiliana na kupata namna bora ya kuboresha maisha ya Wachezaji wakati wote wanapokuwa kazini na wanapostaafu.
Ulega amezitaja taasisi hizo kuwa ni Baraza la Michezo la Taifa- BMT, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi na Chama cha Wachezaji wa Soka Tanzania-SPOTANZA na kuongeza kuwa hali za maisha ya wachezaji zinapaswa kuangaliwa kwa jicho la karibu, kwa sababu wamekuwa na mchango mkubwa katika Taifa.
Ameyasema hayo katika kikao cha pamoja cha wadau wa Taasisi zinazosimamia michezo nchini uliojadili maslahi na namna ya kuwapata Wachezaji wapya, kuanzia ngazi za chini watakaoweza kuendeleza soka la Tanzania.
“Ninaelekeza Idara ya Michezo ya Wizara, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Bodi la Ligi na Chama cha Wachezaji wa Mpira wa Miguu Tanzania- SPOTANZA na wadhamini wetu, mkae mjadiliane kuhusu mustakabali mwema wa Wachezaji wetu ikiwa ni pamoja na huduma za afya na maandalizi ya maisha ya baada ya kustaafu soka” amesema Naibu Waziri Ulega.
Aidha, alizitaka taasisi hizo kusimamia na kuhakikisha Chama cha Wachezaji wa mpira wa miguu Tanzania SPOTANZA kinaimarika ipasavyo kwa kubuni vyanzo vya kudumu vya fedha ili kulinda maslahi ya wachezaji na mchezo wa soka nchini.
“Nawataka pia mshirikiane kwa pamoja katika kubuni vyanzo vya kudumu vya mapato, nataka kwa dhati kabisa kuona chama cha wachezaji wa mpira wa miguu kinaimarika ipasavyo, kuwe na chanzo cha uhakika ambacho kitasimamia vyema haki za wachezaji, leo hii utakuta mchezaji amestaafu lakini maisha yake yanakuwa magumu sana, hii ni kwa sababu hatukuwajengea mazingira mazuri tangu mwanzo,” amesema Naibu Waziri Ulega.
No comments:
Post a Comment