MITIKI ITAKAVYOINUA UCHUMI WA WANANCHI WILAYANI NYASA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 29 March 2021

MITIKI ITAKAVYOINUA UCHUMI WA WANANCHI WILAYANI NYASA

Shamba la mitiki katika kijiji cha Nkali A Kata ya Liluli mwammbao mwa ziwa Nyasa likiwa limetimiza mwaka mmoja
.

Na Albano Midelo, Ruvuma

PROGRAM ya kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu (FORVAC) imetoa ruzuku ya miche ya mitiki 450,000 kwa wananchi  mwambao mwa Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma.

Mratibu wa FORVAC mkoani Ruvuma Marcel Mtunda anasema FORVAC imetumia zaidi ya shilingi milioni 225 kwa ununuzi wa miche ya mitiki  pekee  ambapo mradi huo unatekelezwa katika vijiji vya Nkali A,Liuli,Lipingu na Nkali A wilayani Nyasa.

Anasema miche hiyo inawezesha kupanda hekta zaidi ya 400 na kwamba licha ya program hiyo kukamilika mwaka 2022,FORVAC ina mpango wa kuanzisha vikundi vya uzalishaji wa miche ya mitiki mwambao mwa ziwa Nyasa ili  mradi huo uwe endelevu na kuwanufaisha wananchi.

Kwa upande wake Mratibu wa FORVAC Wilaya ya Nyasa Bugingo Bugingo anasema mtiki unaweza kuvunwa kati ya miaka 15 hadi 20 na kwamba mtiki mmoja wenye mita moja ya ujazo kwa bei ya serikali huuzwa shilingi 800,000/= 

“Watu wasiopungua 10,000 watanufaika na mradi huu kwa wastani ekari moja yenye miti ya mitiki 340 inatarajia kumuingizia mkulima kati ya shilingi milioni 300 hadi 400’’,anasisitiza Mtunda.

Hata hivyo anasema mwananchi ambaye amekusudia kupanda mitiki atafaidika kwa kiasi kikubwa endapo miti hiyo ataitunza vizuri na kwamba mwaka 2018/2019 wakulima walipanda jumla ya mitiki 150,000 katika vijiji vya mradi na mwaka 2019/2020 FORVAC imeleta miche 300,000 ambayo inapandwa hivi sasa na kufanya jumla ya miche iliyotolewa na FORVAC kufikia 450,000.

Hata hivyo anasema katika vijiji vyote vinavyotekeleza mradi huo zinatakiwa kupanda hekta 700 za mitiki na kwamba lengo hilo ni lazima litimizwe kama ilivyokusudiwa  katika vijiji vyote vya ukanda wa mitiki mwambao mwa ziwa Nyasa.

Naye Mwenyekiti Panda Miti Kibiashara  kijiji cha Nkali A Alfonce   Sangana amezitaja ekari za miche ya mitiki ambazo zimepandwa katika kipindi cha mwaka 2020/2021 katika kijiji hicho kuwa ni ekari 58.7 sawa na hekta 23.8 na kwamba miche iliyopandwa ni zaidi ya 26,000.

Hata hivyo anasema katika msimu huo miche iliyorudishiwa ni  miche zaidi ya 15,000 na amewataja wakulima waliopanda mitiki hadi sasa katika kijiji hicho kuwa ni 45.

Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Nkali A Barnabas Mbele ameipongeza serikali kwa kuwaruhusu FORVAC kupeleka mradi wa mitiki mwambao mwa ziwa Nyasa ambapo amesema mradi huo wa miti unakwenda kubadilisha maisha ya wananchi hao kwa kuondokana na umaskini uliokuwepo tangu uhuru.

“Wananchi baada ya kupewa elimu kuhusu faida ya miti ya mitiki,wameupokea mradi kwa moyo mmoja,tuna matumaini makubwa ya kukombolewa kiuchumi miaka michache ijayo’’,anasema Mbele.

Anasisitiza kuwa kutokana na ardhi yenye rutuba ya kutosha iliyopo mwambao mwa ziwa Nyasa ,wakulima wanaweza kuanza kuvuna miti hiyo kati ya miaka kumi hadi 15 hivyo ametoa rai kwa FORVAC kupanua mradi huo  kwenda katika vijiji vingine wilayani Nyasa kwa kuwa ardhi ipo ya kutosha na inafaa kwa uzalishaji wa mitiki.

Mwenyekiti wa Muungano wa Chama  cha Wazalishaji wa miti ya misaji (mitiki) kijiji cha Liuli wilaya ya Nyasa Samwel Mawanja anasema mradi wa mitiki ni mradi pekee ambao haujawahi kutekelezwa tangu uhuru mwambao mwa ziwa Nyasa.

Mawanja anasisitiza kuwa mradi huo unatarajia kuleta tija kubwa kiuchumi kwa wananchi hivyo kuleta mapinduzi makubwa kiuchumi baada ya miti hiyo kuanza kuuzwa.

Ameyataja matarajio ya wananchi hao ambao pia ni wavuvi katika ziwa Nyasa kuwa ni kutengeneza boti za kisasa kwa kutumia miti ya mitiki  hivyo kuwezesha kwenda kuvua mbali badala ya kuendelea kuharibu misitu ya asili kwa kukata miti ya kutengenezea mitumbwi.

Afisa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Bugingo Bugingo kwa mara nyingine tena anatoa rai kwa wananchi mwambao mwa ziwa Nyasa kulinda na kuhifadhi misitu iliyopo kwenye milima ya Livingstone kwa kuacha kulima na kukata miti hovyo.

Anasisitiza kuwa eneo la Mwambao mwa ziwa Nyasa linafaa sana kwa uzalishaji wa mitiki kwa sababu ni eneo ambalo lipo chini ya milima ya livingstone hivyo lina  rutuba nyingi..

Bugingo anayataja miongoni mwa matumizi ya zao la mitiki  ni kutengenezea vitako vya silaha aina ya bunduki,vyombo vya majini kama vile meli na boti na kutengeneza samani mbalimbali zenye gharama kubwa.


Utafiti umebaini kuwa Mahitaji ya mtiki katika soko la duniani ni makubwa ,ndiyo maana nchi za Ulaya na nchi za Asia zikiongozwa na China na India wananunua miti aina ya mitiki kwa wingi kutoka Tanzania,na hata hatujaweza kufikisha hata robo ya mahitaji yao.

Takwimu zinaonesha kuwa Nchi  ya Malyasia kwa mwaka hupata mapato ya Dola  za Marekani zaidi ya bilioni 13 kutokana na kilimo cha mitiki.

Hakuna ubishi mahitaji ya soko la mitiki ni makubwa hivyo wakulima wapya wa mitiki katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na maeneo mengine nchini waongeze uzalishaji wa zao hili,kwa sababu  mahitaji yake yanaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

No comments:

Post a Comment