Anitha Jonas – COSOTA, Dar es Salaam
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameagiza COSOTA na BASATA kuandaa mfumo wa kuuza kazi za Wachoraji na Wachongaji kwa njia ya mtandao. Mheshimiwa Bashungwa ametoa agizo hilo Jijini Dar es Salaam katika kikao chake na Wasanii wa Sanaa ya Uchoraji na uchongaji nchini kilicholenga kutatua changamoto Zinazowakabili katika uendeshaji wa kazi zao ikiwemo suala la masoko.
"Katika karne hii ya 21 suala la Masoko linafanyika kwa njia ya mtandao na njia hii ni rahisi na inatangaza biashara kwa haraka zaidi na katika hili COSOTA mtatakiwa kuhakikisha mnalinda Hakimiliki za kazi hizo," alisema Mhe. Bashungwa.
Akiendelea kuzungumza katika mkutano huo Waziri huyo aliwasihi Wachoraji na Wachongaji kusajili kazi zao COSOTA ili ziweze kulindwa, pia alitoa msisitizo kwa wadau hao kuhakikisha wanawasiliana BASATA pamoja na COSOTA pale wanapokuwa na mikataba yao kibiashara kwa lengo la kupata ushauri wa kisheria ili kuweza kulinda kazi hiyo pamoja na maslahi yake.
Pamoja na hayo naye Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Tanzania (COSOTA) Bibi. Doreen Sinare alieleza kuwa taasisi hiyo imetengeneza Kanuni mpya ambazo zitawasaidia Wachoraji na Wachongaji kunufaika na kazi zao baada ya kuuza kazi zao na kazi hizo kwenda kuuzwa tena nje ya nchi kupitia minada na njia nyingine kama hizo ambapo kazi huuzwa kwa bei za juu ilihali msanii kutokupata chochote kutokana na mauzo hayo zijulikanazo kama ‘resale royalties rights’.
"Napenda kuwasisitiza kuhusu suala la kusajili kazi zenu kuna wakati nilitembelea ofisi za Tingatinga na nikawashauri kuhusu suala la kusajili kazi zenu COSOTA lakini baadhi yenu walikuja ila wengine hawakuja sasa naendelea kuwasisitiza kusajili msisubiri mpaka mnapopata changamoto ndiyo mnaanza kuhangaika," alisema Bibi. Doreen.
Pamoja na hayo Mtendaji huyo alieleza dhamira yake ya kutembelea eneo la biashara ya vinyago Mwenge Machi 19, 2021 kwa lengo la kuwapa elimu ya Hakimiliki na Hakishiriki ili kuwaongezea uelewa wa masuala hayo ikiwemo maboresho ya Kanuni mbalimbali zinazosimamia hakimiliki.
Pamoja na Kituo cha Wachoraji wa Sanaa ya Tingatinga Oysterbay ambapo itakuwa ni mara nyingine anawatembelea. Mbali na hayo Bibi.Doreen alitangaza napenda kutoa ofa kwa wanawake wanaofanya kazi ya Sanaa ya Ufundi kupamba Ofisi ya COSOTA kwa kazi zao ikiwemo kwa Sanaa ya uchoraji au uchongaji
Kufuatia mgogoro wa Tingatinga Arts na Kampuni ya Kenya Mtendaji Mkuu wa COSOTA aliwaelekeza viongozi wa chama hicho kumpeleka mkataba wao katika Ofisi yake ili aweze kutoa ushauri.
Pamoja na hayo Katika kikao Waziri Bahungwa alisisitiza mikataba huo ufuatiliwe na COSOTA, na kama kuna haki za Tingatinga basi haki hizo zifuafuatiliwe na zipatikane hii ni kutokana na sintofahamu ya kusemekana kuwepo kwa baadhi ya wasanii ambao walisaini na kulipwa kwa kazi hiyo. Hivyo mkataba ndio utatoa picha kamili.
Kwa upande Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Bw.Andrian Nyangamale alitoa ombi kwa Serikali kuwa anaomba katika zawadi zile za vinyago au picha za kuchorwa zinazotolewa kwa wageni Ikulu basi Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ataje jina la aliyefanya fanya kazi hiyo pale anapokabishi. *Mh. Waziri alipokea na kuahidi kufanyia kazi jambo hilo.*
No comments:
Post a Comment