WAZIRI BITEKO AKABIDHI GST MAGARI SITA KUIMARISHA UTENDAJI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 1 February 2021

WAZIRI BITEKO AKABIDHI GST MAGARI SITA KUIMARISHA UTENDAJI

Magari sita yaliyokabidhiwa na Waziri wa Madini Mhe. Doto  Biteko kwa Taasisi ya Utafiti wa madini Tanzania (GST) leo Januari 1, 2021Jijini Dodoma. 


Waziri wa Madini Mhe. Doto  Biteko  akikabidhi ufunguo  kwa  dereva  wa moja ya  magari aliyokabidhi kwa Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST) leo  Januari 1, 2021 Jijini Dodoma.

Na Mwandishi wetu- Dodoma

WAZIRI wa Madini Mhe Doto Biteko amekabidhi magari sita yenye thamani ya Shilingi milioni 950 kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ikiwa ni moja ya hatua za Serikali kuimarisha taasisi hiyo. 

 

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi magari hayo leo Januari 1, 2021, Mhe. Biteko amesema dhamira ya Serikali ni kuona mageuzi ya kiutendaji baada kutolewa kwa magari hayo na vifaa vingine vya maabara ambavyo viko hatua za mwisho za manunuzi yake. 

 

"Nakuagiza Mtendaji Mkuu baada ya miezi sita nipate ripoti ya namna magari haya yalivyochangia kuleta tija, kuongeza mapato ya Serikali na kuwahudumia wananchi katika sekta ya madini," alisisitiza Mhe. Biteko 

 

Aidha, amefafanua kuwa Taasisi hiyo ina mchango mkubwa katika kukuza sekta ya madini na kuiwezesha kukuza mchango wake kutoka asilimia tano za sasa hadi kufikia 10 hali itakayowezesha wananchi kunufaika zaidi.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini Mhe. Prof. Shukrani Manya amesema kuwa Serikali inatarajia magari hayo yatatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili yalete matokeo chanya. 

 

“Nawasihi wote watakaotumia magari haya kuzingatia Serikali imewawezesha kupata magari haya ili yawe chachu ya utendaji na si kuyatumia kwa mambo yasiyo ya tija, hivyo tutafuatilia”, alisisitiza Prof. Manya.

 

Naye Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Mussa  Budeba amesema kuwa magari hayo sita na vifaa vya maabara ni chachu ya mageuzi katika utendaji wa Taasisi hiyo na ameahidi kuwa yatatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. 

 

Aliongeza kuwa, Taasisi hiyo inamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuiwezesha kupata magari hayo na vitendea kazi vya kisasa.

 

Magari sita yaliyokabidhiwa ni sehemu ya juhudi za Serikai kuimarisha utendaji wa GST na matumizi sahihi ya vifaa vya kisasa vinavyonunuliwa vitawezesha kuimarisha maabara yake.


No comments:

Post a Comment