Na Faraja Mpina, WMTH
WIZARA ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewakutanisha wadau mbalimbali wa Anwani za Makazi na Postikodi ili waweze kutoa maoni kuhusu ujenzi wa Programu Rununu ya Anwani za Makazi na Postikodi (National Adddressing and Postcode mobile Application-NAPA) unaoendelea kufanyika Mkoani Morogoro na timu ya wataalamu wa TEHAMA kutoka katika Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Utawala wa Wizara hiyo, Kitolina Kippa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amesema kuwa anaamini ujenzi wa programu hiyo utasaidia Sekta mbalimbali katika kufikisha huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi katika maeneo yao ya kijiografia.
“Lengo lililotukutanisha hapa ni kupokea maoni ya programu hii kutoka kwa wadau wetu, kama mjuavyo Wizara yetu ni mtambuka, huduma zetu za mawasiliano zinatumiwa na kila Wizara na taasisi, hivyo tukijifungia sisi wenyewe tunaweza kufanya kitu katika upeo mdogo lakini tukipokea maoni ya watu wengi tukayaunganisha tutatoa kitu kizuri kwa manufaa ya Taifa”, alizungumza Kippa
Aidha, Kippa aliwatia moyo wataalamu wa TEHAMA wanaotengeneza Programu hiyo kuwa ushiriki wao ni muhimu na utaacha sifa na alama katika maisha yao hata kama majina yao yasipotajwa mahali popote bado ni fahari kutambua kuwa walishiriki kutengeneza mfumo ambao watu wanautumia.
Naye Mhandisi Clarence Ichwekeleza Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara hiyo amesema kuwa Wizara imeandaa programu hiyo kwa lengo la kutumia mifumo ya ndani ambayo ni tofauti na ramani za google ‘google maps' ili kuhakikisha wananchi wanatambulika mahali wanapoishi na maeneo wanapofanya kazi au biashara.
“Sote tunafahamu google maps zinatumiwa na huduma za usafirishaji za Uber na Bolt ambapo mara nyingi hazimfikishi mtu mpaka nyumbani, lakini kupitia mfumo huu unaoandaliwa utampeleka mtu mahali husika kwasababu utajumuisha jina la mtaa na namba ya nyumba au jengo husika”, Ichwekeleza
Naye Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku amesema kuwa Sekta nyingi zina mifumo ya kutolea huduma mbalimbali kwa wananchi au ndani ya Serikali ambayo inategemea mifumo unganishi na mifumo ya Utambuzi katika kufanikisha utoaji wa huduma hizo.
Ameongeza kuwa Progamu Rununu ya NAPA imegusa mfumo muhimu sana wa kitaifa ambao ni mfumo wa msingi wa utambuzi wa maeneo unaotegemewa na mifumo mingine ya kutolea huduma kwa jamii.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Mifumo ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango John Sausi amesema kuwa wao kama Wizara wamekuwa wakitengeneza mifumo mbalimbali inayotumika kwenye ukusanyaji wa mapato na malipo Serikalini lakini moja ya vitu ambavyo vimekuwa vikihitajika sana ni mifumo ya utambuzi wa maeneo.
Ameongeza kuwa kwasasa wanatumia google maps ambayo ukiiangalia kwa ujumla wake inaweza kukupoteza kwa sababu haioneshi vipengele muhimu na vya kipekee vinavyotambulisha eneo husika.
“Ni ukweli usiofichika kuwa kama nchi kuna baadhi ya vitu hatuvipati kwa wakati na sababu mojawapo ni kutokuwa na mifumo ya utambuzi wa maeneo ambayo ni muhimu sana kwa taifa letu ili mambo mengine yaendelee na ni msingi wa mifumo mingine kufanya kazi vizuri”, Sausi
Naye Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Palapala amesema kuwa Mamlaka hiyo itakuwa ya kwanza kunufaika na ujenzi wa Program Rununu ya NAPA kwasababu itawezesha kuyatambua na kuyatembelea maeneo ambayo wafanyabiashara wanafanyia biashara zao ili kurahisisha ukusanyaji wa kodi.
Ameongeza kuwa ukosefu wa Anwani za Makazi na Postikodi umekuwa kilio cha Mamlaka hiyo kwa sababu watu wamekuwa wakifanya biashara sehemu ambazo ni ngumu kuwafikia na kuwatambua.
“Kamishna alikuwa ameshaagiza tukutane na watu wa Ardhi na TAMISEMI ili kuona namna ya kuweza kushirikiana kuweka hiki kitu sawa ili kiweze kutusaidia kukusanya mapato, kama ilivyo kwa wenzetu wa benki wana kitu kinaitwa Know your customer(KYC) ili na sisi tuweze kukusanya kodi vizuri tunatakiwa tuwe na Know Your Taxpayer (KYT) tunashukuru Wizara ya Mawasiliano kwa hili na tupo tayari kushirikiana”, amesema Palapala
Kwa upande wa Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Erick Kitali amesema kuwa TAMISEMI ina mifumo anuai ya utambuzi, usimamizi na utunzaji wa taarifa sahihi za maeneo ya utawala ambapo mifumo hiyo ikiunganishwa na huu unaotengenezwa maana yake ni kurahisisha zaidi utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, ameishukuru Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa ushirikishaji kwa sababu mifumo inaanza kuongea baada ya watu kuongea ikiwa ni pamoja na TAMISEMI kutoa wataalamu ambao wapo kwenye timu ya ujenzi wa programu hiyo.
Pamoja na mambo mengine wadau walipitishwa katika hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa program hiyo na kujiridhisha katika vipengele muhimu vya usalama na sera ya usiri ya program hiyo huku wakishauri mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi (National Addressing and Postcode System-NAPS) uunganishwe na Programu Rununu ya NAPA.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
No comments:
Post a Comment