IKUNGI YATEKELEZA AGIZO LA JPM KWA VITENDO YATENGENEZA MADAWATI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 5 February 2021

IKUNGI YATEKELEZA AGIZO LA JPM KWA VITENDO YATENGENEZA MADAWATI

Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung'unyi, wilayani Ikungi mkoani Singida,Yahaya Njiku akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Munkinya, viongozi na wajumbe wa kamati za shule  kabla ya kuwakabidhi madawati yaliyotengenezwa kwa nguvu ya wananchi.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Munkinya  wakiwa kwenye hafla ya kukabidhiwa madawati hayo.

Kaimu Afisa Elimu Kata ya Dung'unyi, Mwalimu Peter Sarumbo,  akizungumza kwenye hafla hiyo.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Dung'unyi  wakiwa kwenye hafla ya kukabidhiwa madawati hayo.

Madawati yakikabidhiwa.

Na Dotto Mwaibale, Ikungi

KATA ya Dung'unyi  katika Halmashauri  ya Wilaya Ikungi mkoani Singida imetekeleza agizo la Rais Dkt.John Magufuli kwa  kutengeneza madawati ili kuwawezesha wanafunzi kukaa kwenye viti wakiwa shuleni.

Akizungumza wakati alimkabidhi madawati hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Yahaya Njiku alisema hatua ya kutengeneza madawati hayo ilifikiwa baada ya Serikali kutoa maagizo ya kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na changamoto ya wanafunzi  kukaa chini.

Njiku alisema kufuatia maagizo hayo ofisi yake  kwa kushirikiana na wananchi  na wazazi walianza mchakato endelevu wa ukarabati wa madawati na kutengeneza madawati mapya zaidi ya 60 ambayo yaligaiwa katika Shule ya Sekondari Munkinya  ambayo ilipata madawati mapya 20 na mengine 40 Shule ya Msingi Dung'unyi.

" Nawaombeni sana kwa umoja wetu huu tuendelee kushirikiana kutengeneza madawati mengine ili kuwaondolea wanafunzi wetu changamoto hii" alisisitiza Njiku.

Njiku alisema Serikali chini ya Rais Dkt. John Magufuli pamoja na kutekeleza Sera ya Elimu bila malipo itaendelea kuweka miundo mbinu bora na rafiki ya wanafunzi kujifunzia.

Katika ziara hiyo ya kukabidhi madawati hayo Njiku aliambatana na Katibu wa Chama cha Mapinduzi  (CCM) wa Kata hiyo, Emanuel Msuta, Kaimu Afisa Elimu Kata,  Mwalimu Peter Sarumbo pamoja na viongozi wa Serikali za Vijiji.

No comments:

Post a Comment