Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Uchukuzi-Uchukuzi, Mhandisi Aron Kisaka, akifafanua jambo kwa wadau (hawapo pichani), wakati wa kikao cha kujadili ada ya leseni za magari maalum ya kukodi, kilichofanyika mkoani Arusha.
Meneja Leseni wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Leo Ngowi, akiwasilisha mada kwa wadau (hawapo pichani) kuhusu ada ya leseni ya magari ya kukodi, uliofanyika Mkoani Arusha.
Mmoja wa Wadau wa Usafirishaji, Brian Fadhili, akifafanua jambo katika kikao cha wadau wa usafirishaji, kilichofanyika Mkoani Arusha. |
WAMILIKI na Madereva wa Magari maalum ya kukodi Mkoani Arusha wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi-Uchukuzi, kuitazama upya ada ya leseni ya magari hayo ya shilingi milioni 1 iliyopendekezwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ili kuwezesha watoa huduma hao kuendelea kufanya biashara.
Wakizungumza katika kikao cha siku moja kilichofanyika mkoani humo cha kujadili ada hiyo wamesema wasafirishaji wengi hawakatai kutoa huduma lakini ni vyema Serikali kupunguza kiwango kwa kufanya utafiti wa kina sokoni.
“Kama watoa huduma tunapenda kuendelea kutoa huduma lakini ada iliyopendekezwa ni kubwa sana kulingana na aina ya biashara tunayofanya na kupitia biashara hii tunaendesha maisha yetu, ikipita hii tunaweza kufunga biashara” amesema Brian Fadhili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji abiria (AKIBOA) mkoani Arusha, Locken Masawe amesema wasafirishaji wanapashwa kujenga hoja ambazo zitaifanya Serikali kufanya maamuzi ya kupunguza au kubakiza ada hiyo.
“Hoja tutakazojenga ndio zitaamua kupunguza au kubakiza ada hiyo maana Serikali hii ni sikivu na inafanya maamuzi kwa kuzingatia maoni ya na ndio maana wako hapa japo wana uwezo wa kufanya maamuzi na ada hii ikabaki kama ilivyo” amesema Masawe.
Masawe ameongeza kuwa Wizara izungumze na halmashauri ya majiji nchini ili kutenga maeneo maalum ambayo magari haya yanaweza kupatikana ili kupunguza changamoto ya kutokuwa kwa watumiaji kujua sehemu za kupata huduma.
Kwa upande wake Meneja Leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Leo Ngowi amesema lengo la Mkutano huo na kusikia maoni ya wadau na kuboresha utoaji wa huduma za usafirishaji nchini.
“Maoni mtakayowasilisha katika Mkutano huu tuangalie maeneo yote yanayohusisha makundi yote yaliyoainishwa tusijikite tu kwenye maeneo machache manake maoni yenu yataborehsa kanuni hizi na kuboresha mazingira ya usafirishaji’ amesema Ngowi.
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Uchukuzi (Uchukuzi) amewahakikishia Wadau hao kuwa maoni yao yatazingatiwa na kufanyiwa kazi kabla ya utekelezaji wake na kuwasisitiza wasafirishaji kutoa maoni kwa maandisi kupitia barua pepe ya Katibu Mkuu-Uchukuzi ili kuharakisha mchakato huo.
Imetolewa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
No comments:
Post a Comment