MKUTANO WA KIMATAIFA WA ELIMU BORA KUFANYIKA KUANZIA APRILI 20, 2021 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 31 January 2021

MKUTANO WA KIMATAIFA WA ELIMU BORA KUFANYIKA KUANZIA APRILI 20, 2021

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga (kushoto) akizungumza na wanahabari juu ya Mkutano wa Kimataifa wa elimu bora unatarajia kufanyika Tanzania jijini Dar es salaam kuanzia Aprili 20 hadi 22, 2021. Kulia ni Ofisa Utetezi wa TEN/MET, Bi. Nasra Kibukila akifuatilia mkutano huo.


Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga (kushoto) akizungumza na wanahabari juu ya Mkutano wa Kimataifa wa elimu bora unatarajia kufanyika Tanzania jijini Dar es salaam kuanzia Aprili 20 hadi 22, 2021. Kulia ni Ofisa Utetezi wa TEN/MET, Bi. Nasra Kibukila akifuatilia mkutano huo.

MKUTANO wa Kimataifa wa elimu bora unatarajia kufanyika Tanzania jijini Dar es salaam kuanzia Aprili 20 hadi 22, 2021 huku ukibeba ujumbe wa mwaka huu kwamba, “Uwajibikaji wa pamoja katika kugharamia elimu bora”. Mkutano huo unatarajia kushirikisha wawakilishi wa mabunge ya Afrika, Wadau wa Maendeleo, Wanazuoni, Bodi za mikopo za elimu ya juu, Vyama vya walimu, Sekta binafisi, Sekta za mawasiliano, Wizara ya Elimu Sayansi na Tekinolojia (MoEST), TAMISEMI, Vyuo vya Ufundi, Wazazi, Wanafunzi na wadau wengine.  

Akizungumza na wanahabari juzi jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga alisema pamoja na mambo mengine mkutano huo mkubwa wa elimu unatarajiwa kujadili mada anuai zikiwemo mchango wa wadau wa maendeleo katika kuboresha ubora wa elimu Tanzania, Matumizi ya Tekinolojia katika kujifunza na kufundisha ili kuboresha elimu zaidi.

Alisema wadau wa elimu pia watajadili Mchango wa serikali katika kuimarisha elimu nyakati za maafa ikiwemo magonjwa ya mlipuko mfano COVID-19, Hatima ya elimu ya juu: Kwanini watahiniwa wengi hawaajiriki na masuala mengine ya elimu lengo ikiwa ni kuhakikisha kunakuwemo na maboresho na maendeleo yanaochagizwa na wadau wa sekta hiyo.

Aidha alisema mada husika zitawasilishwa na wataalam kabla ya washiriki kuanza kujadiliana katika mkutano huo, huku akiweka bayana kuwa ujumbe wa mwaka huu umelenga kuchochea na kutoa hamasa kwa wadau wa elimu ndani na nje ya Tanzania kuwajibika kwa pamoja kushirikiana na serikali katika kuboresha na kuwezesha utoaji wa elimu bora katika kufikia malengo ya maendeleo endelevuifikapo 2030. 

"...Mkutano huu wa kimataifa utarajia kuwa na wadau mbali mbali ndani na nje ya Tanzania wakiwemo; Wawakilishi wa mabunge ya Afrika,Wadau wa Maendeleo, Wanazuoni, Bodi za mikopo za elimu ya juu, Vyama vya walimu, Sekta binafisi, Sekta za mawasiliano, Wizara ya Elimu Sayansi na Tekinolojia (MoEST), TAMISEMI, Vyuo vya Ufundi, Wazazi, Wanafunzi nk," alisisitiza Bw. Wayoga.

Aliongeza kuwa mtandao wa TEN/MET unapenda kutoa rai kwa wadau wa elimu ndani na nje ya nchi, kushiriki katika mkutano huo wa kimataifa ili kuweza kujifunza njia na mbinu mbalimbali zinazoweza kutumika katika kuendelea na kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia. 

Hata hivyo, Bw. Wayoga aliongeza kuwa mkutano huo utaendeshwa katika mfumo wa mijadala, ambapo mada mbalimbali zinazohusiana na elimu zitajadiliwa ili kutoa fursa kwa wadau kujadiliana zaidi. Na kutakuwa na uwasilishaji wa tafiti za kielimu wenye lengo la kuufahamisha umma hali na mwenendo wa elimu ya Tanzania kuanzia ngazi ya elimu ya awali, elimu ya msingi, sekondari hadi chuo kikuu. 

Kwa miaka kumi na moja sasa, TEN/MET imekuwa ikiandaa mkutano wa kutathimini na kujadili utolewaji wa elimu ubora nchini Tanzania. Katika mkutano huu, TEN/MET imekuwa ikiwashirikisha wadau mbalimbali wa elimu katikakufanya tathmini nakujadili changamoto katika utolewaji wa elimu bora nchini na kwa pamoja kuazimia mapendekezo ya nini kifanyike katika kutatua changamoto zinazoathiri utoaji wa elimu bora. Ama kwa hakika mkutano huu umekuwa ukileta tunu katika sekta ya elimu na kwa wadau wa elimu kwa ujumla. 

"...Tunapenda kutoa wito na kuwakaribisha wadau mbali mbali wa elimu kuungana nasi kwa kushiriki katika mkutano huu wa kimataifa utakaojadili taswira ya elimu Tanzania," alibainisha Mratibu wa TEN/MET, Bw. Wayoga kwa wanahabari alizungumzia mkutano huo.


Baadhi ya wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakiwa katika mkutano na Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga, uliofanyika ofisi za TEN/MET jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment