WIZARA YA KILIMO imesema
itahakikisha wakulima wa wilaya ya Tarime na mkoa wote wa Mara wanapata mbegu bora za mahindi na mbolea
kwa bei elekezi ya serikali ili kudhibiti biashara ya magendo mpakani.
Kauli
hiyo ya serikali imetolewa Novemba 21.2020 na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Gerald Kusaya alipozungumza na wakulima na wananchi wa kijiji cha Nyamwaga
wilaya ya Tarime wakati alipokagua mashamba darasa ya kahawa,mihogo na migomba.
Kusaya
alisema hayo kufuatia malalamiko ya wakulima wa Tarime kusema hawapati mbegu
bora za mahindi na mbolea zinazozalishwa nchini hali inayowafanya wategemee
bidhaa hizo toka nchini Kenya zinazoingizwa kinyemelea mpakani Sirari.
Akizungumzia
suala la uhaba wa mbegu na mbolea Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhandisi Mtemi
Msafiri alimweleza Katibu Mkuu huyo kuwa wakulima wanapata shida ya kupata
pembejeo za serikali na kuwa Tarime hazifiki hali inayowafanya wakulima
kushindwa kuzalisha kwa tija mazao hususan mahindi yanayotegemewa kwa chakula.
“Tuna
shida kubwa ya mbegu bora za mahindi hapa Tarime na zinazopatikana zinauzwa bei
kubwa mfano kilo mbili kwa shilingi 15,000 na nyingi zinatoka nje ya nchi “alisema Mhandisi Msafiri
Katibu
Mkuu Kusaya aliwahakikishia wakulima hao kuwa wizara yake kupitia Wakala wa
Mbegu (ASA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) utafikisha mbegu za mahindi
na alizeti pia mbolea mkoani humo mapema kabla ya Desemba mwaka huu .
“Nimeagiza
Mtendaji Mkuu wa ASA Dkt. Sophia Kashenge afike hapa Mara na ahakikishe mbegu
bora za mahindi zinauzwa kwa bei elekezi ya serikali ili wakulima wengi wamudu
na kutoendelea kuumizwa na wafanyabiashara. Mbegu hizi zitauzwa chini ya shilingi
10,000 “alisema Kusaya hatua iliyopokelewa kwa shangwe na wakulima.
Kusaya
aliongeza kuwaeleza wakulima hao kuwa tayari ameelekeza mbolea iletwe mapema
kabla ya Desemba na Malmaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na kuwa iwafikie
wakulima kwa bei elekezi ya serikali.
“Niwasihi
wakulima wangu muwe na subira kabla ya Desemba mwaka huu TFRA wataleta mbolea
hapa Tarime na mkoa wote wa Mara itakayouzwa kwa bei elekezi “alisisitiza
Kusaya.
Akiwa
kijijini Nyamwaga kwenye mkutano wa hadhara wakulima walieleza kuwa wanauziwa
mbolea aina ya NPK mfuko wa kilo 50 kwa bei ya Shilingi 60,000 hadi 80,000 kwa
inayotoka Kenya na ya Tanzania kwa Shilingi 80,000 hadi 100,000 hivyo kushindwa
kumudu.
Katika
hatua nyingine Kusaya aliwashauri wakulima wa wilaya ya Tarime pamoja na kulima
mazao ya chakula wajikite pia kuzalisha mazao ya kahawa, chai na migomba
yanayostawi vema kutokana na hali ya hewa nzuri na kuwa wizara yake itatoa
utaalam na pembejeo ikiwemo mbegu bora.
Kusaya
aliongeza kuwahakikishia wakulima wa migomba na mihogo kuwa tatizo la wadudu
wasumbufu litapatiwa suluhisho mapema kupitia taasisi ya Utafiti wa kilimo
(TARI) ambapo watafiti watafika Tarime na Butiama kukutana na maafisa ugani na
wakulima
“Niwatoe
hofu wakulima wa mihogo na migomba kuhusu tatizo la ugonjwa unaoharibu mazao
hayo, kuwa wiki ijayo wataalam toka TARI Maruku (Bukoba) na wale wa TARI
Ukirigulu (Mwanza) watafika hapa Tarime kutatua changamoto za magonjwa haya kwa
kuwafundisha maafisa ugani namna ya kukabiliana na wadudu hawa” aliahidi Katibu
Mkuu Kusaya.
Ili
kuhakikisha wakulima wanapata elimu na teknolojia ya kuwasadia kutatua
changamoto za kilimo, Katibu Mkuu huyo wa kilimo alitoa agizo kwa wakurugenzi
wa halmashauri nchini kuacha kuwatumia maafisa ugani kwenye kazi za utawala ikiwemo
kazi ya utendaji wa vijiji na kata.
“Hawa
maafisa ugani wameajiliwa kwenda shambani hivyo wasipangiwe kukaimu utendaji wa
vijiji au kat. Tunataka kila kijiji kiwe na afisa ugani kuwasaidia wakulima
kutatua changamoto za mazao yao” alisema Kusaya.
Katibu
Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Mara
kwa kutembelea wilaya za Musoma, Butiama na Tarime ambapo amekutana na kufanya
mazungumzo na wakulima pamoja na kukagua shughuli za kilimo mashambani.
No comments:
Post a Comment