SIDO YAZITAKA HALMASHAURI KUSHIRIKIANA NA CAMFED KUWAWEZESHA WASICHANA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 27 November 2020

SIDO YAZITAKA HALMASHAURI KUSHIRIKIANA NA CAMFED KUWAWEZESHA WASICHANA

Mgeni rasmi kwenye Mkutano wa Mwaka Kitaifa wa Shirika la CAMFED, Meneja Mafunzo wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo nchini Tanzania (SIDO), Bw. Stephen Bando (kulia) aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa SIDO akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Ukumbi wa Msimbazi Center jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya CAMFED, Bi. Jeanne Ndyetabura akifuatilia hotuba ya mgeni rasmi.



Mwenyekiti wa Bodi ya CAMFED, Bi. Jeanne Ndyetabura (kushoto) akipokea zawadi ya moja ya bidhaa zilizoongezwa thamani na wasichana wajasiriamali waliowezeshwa na Shirika la CAMFED walipotembelea maonesho ya bidhaa kwenye Mkutano wa Mwaka Kitaifa wa Shirika la CAMFED, uliofanyika Msimbazi Center.


Mgeni rasmi kwenye Mkutano wa Mwaka Kitaifa wa Shirika la CAMFED, Meneja Mafunzo wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo nchini Tanzania (SIDO), Bw. Stephen Bando (kulia) aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa SIDO akitembelea maonesho ya bidhaa kwenye Mkutano wa Mwaka Kitaifa wa Shirika la CAMFED, uliofanyika Msimbazi Center. Walioambatana naye ni Mwenyekiti wa Bodi ya CAMFED, Bi. Jeanne Ndyetabura pamoja na Mkurugenzi wa CAMFED, Lydia Wilbard.

Mgeni rasmi kwenye Mkutano wa Mwaka Kitaifa wa Shirika la CAMFED, Meneja Mafunzo wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo nchini Tanzania (SIDO), Bw. Stephen Bando pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya CAMFED, Bi. Jeanne Ndyetabura wakitembelea maonesho ya bidhaa kwenye Mkutano wa Mwaka Kitaifa wa Shirika la CAMFED, uliofanyika Msimbazi Center.


Mmoja wa wanufaika wa Shirika la CAMFED, Bi. Eva John akielezea CAMFED ilivyomuwezesha katika kilimo cha nanasi na alianza na heka moja lakini sasa amefanikiwa kufikisha hekari sita za shamba la mananasi.

Na Joachim Mushi, Dar

SHIRIKA la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo nchini Tanzania (SIDO) limeziomba halmashauri zenye miradi ya Shirika la CAMFED inayowasaidia na kuwawezesha wasichana kielimu na uchumi kutoa ushirikiano ili kufanikisha miradi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Meneja Mafunzo wa SIDO, Bw. Stephen Bando alipokuwa akifungua Mkutano wa Mwaka Kitaifa wa Shirika la CAMFED, ulioshirikisha wasichana wanufaika na miradi anuai ya CAMFED.

“…Nitoe wito kwa kurugenzi tendaji za halmashauri na kamati za wilaya za CAMFED kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya CAMFED inayoendelea kwa wasichana ili iweze kuleta tija zaidi kwa mtandao wa CAMA na kwa jamii kwa ujumla,” alisema Bw. Stephen Bando.

Pamoja na hayo alitoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano wa CAMFED kwa kuwasaidia vijana kwani vijana ni nguvu kazi muhimu kwa maendeleo ya taifa la leo na la kesho.

Aidha alisisitiza kuwa, Shirika la SIDO litaendelea kushirikiana na CAMFED ili kuhakikisha miradi ya kuwasaidia wasichana hao kupata elimu ya ufundi na ujuzi inafanikiwa zaidi na kuwa na tija ili kundi hilo la vijana liweze kujitegemea.

“…Naomba kuwashukuru sana Shirika la CAMFED na kuwaomba wadau wengine ili kuhakikisha wasichana wanapata fursa za kielimu, kiujuzi, ufundi, mafunzo ya biashara, mikopo ya elimu ya juu, pamoja na kupata shughuli za kujitegemea ili waweze kujikomboa kiuchumi,” alisema Bw. Bando.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya CAMFED, Bi. Jeanne Ndyetabura akizungumza katika mkutano huo, alisema shirika hilo tayari limesaidia wasichana 1193 Kwenye mitaji na mikopo yenye thamani ya sh 1,007,120,000/- kutoka wilaya 32 za mradi ndani ya mikoa 9, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda.

Hata hivyo, alibainisha kuwa CAMFED imetoa mafunzo ya biashara na mbinu mbalimbali za kujikwamua kiuchumi kwa kushirikiana na wadau ikiwemo SIDO na wadau wa halmashauri kwenye halmashauri wanazofanya miradi.

Awali akitoa ushuhuda, katika kuwezeshwa kibiashara msichana Bi. Eva John aliwataka vijana hasa wa kike kutokata tamaa katika kupambana kujikwamua kiuchumi kwani yeye akiwezeshwa na CAMFED alianza kilimo cha nanasi na heka moja lakini sasa amefanikiwa kufikisha hekari sita. "...Ushauri wangu kwa vijana wenzangu ni kwamba tusikate tamaa wanawake au wasichana tunaweza ukithubutu unaweza, tuanzishe kile ambacho tunaona tunaweza kukifanya na hatimaye kwa jitihada tunaweza kufikia malengo yetu...," alisisitiza Bi. Eva John ambaye kwa sasa ni mkulima mzuri wa mananasi Chalinze. 

Mkutano huo ulikwenda sambamba na uzinduzi wa program maalum ya kuwawezesha wasichana kiongozi wa biashara ambao watakwenda kutoa elimu zaidi kwa wasichana katika kata zao na kujikuta kundi kubwa la mabinti wakinufaika kwa kuwa wajasiriamali hivyo kujikwamua kiuchumi na pia kuchangia pato la taifa.


Mmoja wa wanufaika wa Shirika la CAMFED, akielezea CAMFED ilivyomuwezesha katika kilimo cha nanasi na alianza na heka moja lakini sasa amefanikiwa kufikisha hekari sita za shamba la mananasi.

Baadhi ya washiriki Mkutano wa Mwaka Kitaifa wa Shirika la CAMFED, wakifuatilia mada anuai zikiwasilishwa katika mkutano huo.

Meneja Miradi wa CAMFED, Anna Sawaki (kushoto) akizungumza na washiriki Mkutano wa Mwaka Kitaifa wa Shirika hilo.

No comments:

Post a Comment