MIUNDOMBINU YABORESHWA HALMASHAURI YA MJI NEWALA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 4 November 2020

MIUNDOMBINU YABORESHWA HALMASHAURI YA MJI NEWALA

Ujenzi wa Barabara ya Kiduni – Makondeko - Mkunya kwa kiwango cha Lami yenye urefu wa Km 1 inayojengwa na TARURA katika Halmashauri ya Mji wa Newala mkoani Mtwara kwa lengo la kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa eneo hilo.

Na Bebi Kapenya

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Halmashauri ya Mji wa Newala mkoani Mtwara umeendelea kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa kujenga miundombinu ya barabara na vivuko katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Meneja wa TARURA Halmashauri ya Mji wa Newala Mhandisi Dickson Mkokota alisema, ujenzi wa Barabara ya Kiduni – Makondeko - Mkunya kwa kiwango cha Lami yenye urefu wa Km 1 utasaidia kurahisisha usafiri na kufikia kwa urahisi huduma za kijamii kwasababu barabara hiyo ni njia inayoelekea moja kwa moja kwenye chanzo kikuu cha maji yanayotumiwa na wananchi wote wa Newala.

“Ujenzi wa Barabara hii utagharimu zaidi ya Shilingi Milioni 400, barabara itakuwa na mifereji ya kukusanya maji, makaravati na vivuko vidogo vinavyoingia kwenye mitaa hasa maeneo ya nyumba za ibada ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wa eneo hili waweze kusafirisha mazao yao kwa urahisi,” alisema Meneja huyo.

Naye, Bw. Shekhe Mpota Mkazi wa Newala ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara hiyo itakayoleta unafuu mkubwa sana kwa wananchi ambayo itapelekea kusafirisha mazao yao kwa urahisi ikiwemo korosho, mbaazi na ufuta.

“Tunaishukuru  Serikali kwa ujenzi wa barabara hii kwasababu itatuondolea kero ya kusafirisha mazao yetu hasa korosho kwavile korosho zote za Newala mjini zinatoka mashambani ambapo barabara hii inaelekea na kuja huku mjini hivyo, barabara hii ikikamilika itatusaidia sana wananchi kusafirisha mazao yetu na kufanya biashara kwa urahisi, pia ni njia rahisi ya  kufika mpakani mwa Msumbiji kwa kupitia Mto Ruvuma”, alisema Bw. Mpota

Aidha, mbali na utekelezaji wa mradi huo  TARURA katika  Halmashauri ya Mji wa Newala imekamilisha ujenzi wa Barabara ya Elimu kiwango cha Lami yenye urefu wa km 1 katika eneo la Nangwala, imefanya matengenezo ya barabara za Newala mjini kwa kuchonga barabara kwenye makazi ya wananchi eneo la PCCB Km 16 ambazo tayari zimeshakamilika na imekamilisha ujenzi wa Korongo eneo la Julia lenye urefu wa mita 150 na upana usiopungua mita 3 ambapo kwa mujibu wa Meneja huyo  korongo hilo limesaidia kupunguza kero kwa wananchi  kutokana na maji ya mvua yaliyokuwa yanaathiri makazi ya watu na mashamba.

‘‘Barabara zetu nyingi zinaathirika na maji ya mvua, maji mengi yanayotoka Newala mjini yalikuwa yanaathiri sana makazi ya watu na mashamba, kutokana na ujenzi wa Korongo hili tumefanikiwa kukusanya maji yote yanayotoka mjini kushukia kwenye hili korongo na hatimae yanaelekea mto Ruvuma, kiufupi hili korongo limesaidia kupunguza kero kwa wananchi wa Newala mjini,” alisema Mhandisi Mkokota.

Wakala wa Barabara za Vjijini na Mijini (TARURA) katika Halmashauri ya Mji wa Newala unahudumia Mtandao wa Barabara wenye urefu wa Km 406 na jitihada za uboreshaji wa huduma za usafiri na usafirishaji ili kuinua uchumi wa wananchi zinaendelea.

No comments:

Post a Comment