Umati mkubwa wa watu wakihudhuria mazishi ya Maradona. |
Baadhi ya mashabiki walipiga makofi wengine wakilia walipokuwa wakipita karibu na jeneza la Maradona. |
MWANASOKA, Diego Maradona amefanyiwa mazishi katika sherehe ya kibinafsi katika mji wa Buenos Aires nchini Argentina siku moja baada ya kufariki dunia. Jamaa na marafiki wa karibu tu ndio waliohudhuria mazishi yake.
Lakini awali, kundi kubwa la watu lilijitokeza kutoa heshima zao za mwisho wengi wakiwa wanabubujikwa na machozi na kuonesha upendo. Maradona alifariki dunia kwasababu ya mshtuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 60. Kifo chake kimesababisha watu kumuombeleza kote duniani lakini hakuna walioomboleza kama raia wa nchi yake waliomchukulia kama shujaa wa taifa.
Jeneza la Maradona lilifunikwa bendera ya taifa na fulana ya mpira nambari 10 nafasi aliyocheza uwanjani - pia fulana hiyo ilikuwa inaoneshwa kwa umma katika makao ya rais. Kufikia mchana, foleni ya waliokuwa wamekuja kutoa heshima zao za mwisho ilifika umbali wa zaidi ya kilomita moja na polisi ikakabiliana na waombolezaji walipokuwa wanajaribu kufunga kwasababu ya muda.
Aidha, kulikuwa na taarifa za waombolezaji kurushiwa mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira. Mmoja wa waombolezaji aliona ni kana kwamba polisi wametumia nguvu kupitia kiasi.
"Tumepanga foleni bila fujo yoyote na ghafla polisi wakaanza kurusha risasi za mpira," anasema, akinukuliwa na shirika la habari la Reuters. "Haifai, Mimi nataka tu kumuaga Diego kwa mara ya mwisho."
Na hatimaye mamlaka haikuwa na budi zaidi ya kufunga zoezi la kuruhusu raia kutoa heshima zao za mwisho ili kudumisha amani. Gari iliyokuwa imebeba mwili wake ilielekea eneo la makaburi la Bella Vista viungani mwa mji ambapo alizikwa kando na wazazi wake. Katika klabu ya Napoli ambapo Maradona alicheza kwa miaka saba na kubadilisha kabisa klabu hiyo, mashabiki walimiminika katika uwanja wa klabu hiyo kutoa heshima zao za mwisho wakiwa wanapaza sauti na kutaja jina lake "Diego, Diego!".
Kwa siku ya pili raia walikuwa wanakiuka kanuni zilizowekwa za kukabiliana na virusi vya corona ili waweze kutoa heshima zao za mwisho kabla ya mechi ya Ligi ya Europa iliokuwa imepangwa kati ya Napoli dhidi ya timu ya Rijeka ya Croatian. Timu ya Napoli ambayo wachezaji wake wote walijitokeza uwanjani wakiwa wamevaa bangili nyeusi ya mkono na jezi nambari 10 mgongoni, ilishinda mechi hiyo mabao mawili kwa nunge.
"Alikuwa wa kipekee, aliwakilisha kila kitu, kila kitu kwetu sisi wakaazi wa Naples, shabiki Gianni Autiero amezungumza na shirika la habari la Reuters. "Maishani mwangu nimelia kwasababu ya watu chache sana na Diego ni mmoja wao."
Mmoja wa wachezaji ambaye mchezo wake ulisifika kuwa bora siku zote, Maradona, maisha yake ya kibinafsi yalikumbwa na utata wa utumiaji dawa za kulevya na pia uraibu wa pombe. Mapema Novemba, Maradona alifanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe kwenye ubongo ambao ulifanikiwa na alikuwa amepangiwa kutibiwa tatizo la utegemezi wa pombe.
Matokeo ya awali ya uchunguzi wa kifo chake yanaonesha kuwa alipata "matatizo la moyo".
Mchezaji huyo wa Argentina aliyekuwa mshambuliaji kiungo wa kati na kocha wa timu hiyo alifariki dunia nyumbani kwake Tigre, karibu na mji wa Buenos Aires. Wa mwiso kumuona Maradona akiwa hai alikuwa mpwa wake Johnny Esposito, kulingana na taarifa za.
Maradona alijaaliwa kupata watoto watano na aliyekuwa mke wake, Claudia Villafane, 58, ambaye walitengana mwaka 2004 baada ya miaka 20 ya ndoa.
-BBC
No comments:
Post a Comment