MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma amewahakikishia wananchi wanaoishi kwenye mlima Uluguru kuwa hawatashushwa bali watafundishwa njia na mbinu bora za kuishi milimani kama wanavyofanya watu wa Lushoto na kwingine duniani.
Fikiri aliyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni ya udiwani kwenye Kata ya Magadu ambayo sehemu ya jamii ya watu wa kata hiyo wanaishi kwenye mlima Uluguru na kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji.
“ Tumezielekeza Taasisi mbalimbali za misitu kuacha kwenda kupanda miti kwenye mlima huo badala yake miti hiyo ipandwe na wananchi wa maeneo hayo ili waweze kuitunza tofauti na sasa ambapo miti inayopandwa inakauka kwakuwa wananchi hao wanaona sio sehemu yao na hivyo kukauka” alisema Fikiri.
Akimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo Juma Kiduka, Mwenyekiti huyo wa CCM Manispaa ya Morogoro alisema Serikali ya CCM inajenga viwanda nchi nzima sio tu kutoa ajira bali kuwezesha Wakulima wa Morogoro na nchi nzima kupata Soko la uhakika wa mazao yao.
“ Hapo Mkambarani kwa pembeni kuna kiwanda cha mfano cha kusindika mazao ya mikunde kwenye mkoa wetu kitasaidia sana kuinua maisha ya wakulima wa mazao hayo ya mikunde na ajira kwa vijana na mama zetu” aliongeza Fikiri.
Alisema kitendo cha kwenda kuuza mali ghafi nchi za nje kunapeleka ajira pia kwa watu wa nje lakini viwanda vikiwa hapa nchini vitatoa ajira hizo kwa vijana na watanzania na hivyo kusaidia kuchichea maendeleo ya Taifa hili ambalo asilimia zaidi ya 70 ya wananchi wale wanategemea kilimo.
Amebainisha kuwa ilani ya CCM ya miaka mitano 2015 hadi 2020 imetekelezwa kwa asilimia 100 ndio maana Chaka kinampa nafasi nyingine ya kusimamia ilani ya CCM kwa miaka mingine mitano na hakuna ubishi kuwa atashinda kwa kishindo.
Fikiri alisema kazi iliyopo mbele ya Wana Morogoro mjini kesho kutwa ni kumchagua Azizi Abood kuwa Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kiduka kuwa Diwani wa Kata ya Magadu na Rais John Pombe Magufuli kuwa Rais wa awamu ya sita ili amalizie kazi kubwa aliyoianza ya kuleta maendeleo ya Tanzania.
Kwa upande wake Mgombea Udiwani wa Kata ya Magadu Juma Kiduka alisema kuna kazi kubwa inafanywa na serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kuleta maendeleo ya Kata ya Magadu na Jimbo la Morogoro mjini hivyo kama mtumishi wao anakwenda kusimamia miradi hiyo ili maendeleo yafikiwe.
Akizungumzia changamoto ya maji alisema tayari kuna Mradi Mkubwa wa maji unaendelea kwa sasa na utakapokamilika utatatua changamoto zote za maji kwenye kata na Jimbo la Morogoro mjini hivyo waendelee kuiamini CCM maana sera zake zinatekelezeka.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo aliyekuwa Meya wa Zamani wa Manispaa ya Morogoro Profesa. Romanus Ishengoma amewataka wakazi wa kata hiyo kumuamini Rais John Pombe Magufuli na wagombea wa CCM Kwani amefanya kazi kubwa katika Historia ya Tanzania.
“Mimi mnadhani nipo CCM kwa bahati mbaya? Simnajua nina akili kubwa sio? nipo CCM kwakuwa nina uhakika na kazi za CCM, Sera zake na wagombea wake” alisisitiza Ishengoma.
Kampeni zinaendelea kupambana Moto katika dakika za lala salama zikiwa imebaki siku moja tu kabla ya Wananchi wa Tanzania kupiga kura kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani.
No comments:
Post a Comment