WAHANDISI 264 WACHUKULIWA HATUA KUKIUKA MAADILI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 1 September 2020

WAHANDISI 264 WACHUKULIWA HATUA KUKIUKA MAADILI

Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mhandisi Patrick Barozi, akifafanua jambo wakati uongozi wa bodi hiyo ulipokutana na waandishi wa habari kuzungumzia kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wahandisi yanayotarajiwa kufanyika tarehe 3 na 4 mwezi Septemba, 2020 jijini Dodoma.



Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya maadimisho ya Siku ya Wahandisi kwa mwaka huu, Profesa Bakari Mwinyiwiwa, akisisitiza jambo wakati uongozi wa bodi hiyo ulipokutana na waandishi wa habari kuzungumzia kuhusu maadhimisho ya siku hizo yanayotarajiwa kufanyika tarehe 3 na 4 mwezi Septemba, 2020 jijini Dodoma.


BODI ya Usajili wa Wahandisi (ERB), imesema kuwa imechukua hatua kwa wahandisi 264 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 kutokana na makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa maadili ya taaluma ya kiuhandisi ambayo ni kinyume na kiapo chao.

Hayo yamesemwa na Msajili wa Bodi hiyo Mhandisi Patrick Barozi, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusiana na maadhimisho ya Siku ya Wahandisi kwa mwaka huu ambayo yatafanyika jijini humo tarehe 3 na 4 Mwezi Septemba.

Mhandisi Barozi, amefafanua kuwa hatua hiyo huchukuliwa na bodi hiyo  mara tu baada ya wahandisi hao kula kiapo cha utii ambacho kinawakumbusha kuwajibika vyema kwenye taaluma zao na maamuzi yao ya utendaji wao wa kihandisi wa kila siku.

“Bodi imechukua hatua mbalimbali  kwa wahandisi 264 ikwemo kuwaonya na kuwapeleka mahakamani wahandisi ambao walionekana kukiuka kiapo chao cha utii katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na itaendelea kufuatilia wahandisi ambao hawana maadili lengo ni kuhakikisha wahandisi wanazingatia maadili ya taaluma yao siku zote”, amefafanua Barozi.

Kuhusiana na siku hiyo ya wahandisi Mhandisi Barozi amesisitiza kuwa mbali na kuwa na shughuli mbalimbali zitakazofanywa, pia wataalamu watakula kiapo cha utii kama ilivyo kwa miaka mingine ili kufanya wawajibike vyema kwenye taaluma zao.

Aidha, ametaja shughuli nyingine zitakazofanyika ni pamoja na kuwepo kwaa kongamano la wahandisi vijana, majadiliano ya kitaaluma, maonesho mbalimbali ya ubunifu na teknolojia na biashara, kutoa tuzo mbalimbali kwa awahandisi na makampuni , kuwatambua na kuwazawadia wahandisi wahitimu waliofanya vizuri katika mitihani yao ya mwaka wa mwisho wa 2019/2020.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya maadhimisho ya Siku ya Wahandisi, Profesa  Bakari Mwinyiwiwa amesema kuwa lengo kuadhimisha siku ya wahandisi ni kuuwezesha umma kutambua michango chanya inayofanywa na wahandisi wa Tanzania katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Ametanabaisha kuwa lego jingine ni kuwatambua wahandisi hao, makampuni na mashirika ya kihandisi yaliyotoa michango mikubwa ya kihandisi katika maendeleo ya Taifa na hivyo kuwahamasisha wahandisi wengine kufanya shughuli zao vizuri zaidi.

Maadhimisho ya Siku ya wahandisi Tanzania kwa mwaka huu ambayo yanafanyika kwa mara ya 17 tangu kuanzishwa kwake yanatarajiwa kushirikisha wahandisi zaidi ya 5000 kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo Zimbabwe, Kenya, Nigeria, Uganda, Rwanda, Misri, Malawi, Botswana na Kenya.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.


No comments:

Post a Comment