TMA YATOA MWELEKEO MSIMU WA MVUA OKTOBA – DISEMBA, 2020 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 8 September 2020

TMA YATOA MWELEKEO MSIMU WA MVUA OKTOBA – DISEMBA, 2020

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi (katikati) akizungumza alipokuwa akitoa kwa wanahabari utabiri wa mwelekeo wa msimu wa mvua kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2020 jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi (katikati) akizungumza alipokuwa akitoa kwa wanahabari utabiri wa mwelekeo wa msimu wa mvua kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2020 jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Huduma za Utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Hamza Kabelwa akifuatilia.


Na Joachim Mushi

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa mwelekeo wa msimu wa mvua kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2020 huku ikiainisha uwepo wa mvua za chini ya wastani hadi wastani karibuni maeneo yote yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.

Akitoa utabiri huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi amesema sehemu zitakazo kubwa na hali hiyo, ni maeneo mengi ya ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya Kaskazini pamoja na maeneo ya Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Alisema Kanda ya Ziwa Viktoria, maeneo ya Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma mvua zinatarajiwa kunyesha kwa kiwango cha chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ambazo pia zinatarajiwa kuambatana na vipindi virefu vya ukavu. 

"...Mvua hizi zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya mwezi Septemba, 2020 katika mkoa wa Kagera na kutawanyika katika mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Simiyu, Shinyanga na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma katika wiki ya tatu ya mwezi Septemba, 2020 na zinatarajiwa kuisha mwezi Januari, 2021."

Aliongeza kuwa, kwa ukanda wa Pwani ya Kaskazini, katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Kaskazini mwa Morogoro, mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kunyesha kwa kiwango cha chini ya wastani hadi wastani na zinatarajiwa kuchelewa kidogo na kuanza katika wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2020 na kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Disemba. Mvua za Vuli pia zinatarajiwa kuambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi. 

Aliitaja mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara kuwa inatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi, ambazo zinatarajiwa kuanza kwa kuchelewa pia katika wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2020. Na zinatarajiwa kuisha mwezi Januari, 2021. 

Aidha akitoa ushauri alisema upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi, pamoja na visumbufu vya mazao na magonjwa vinatarajiwa kuongezeka, hivyo kuzitaka mamlaka husika kuchukua tahadhari na kuwashauri vizuri wakulima na wadau wengine wanaoguswa.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, wakulima wanashauriwa kupanda mbegu na mazao yanaweza kukomaa ndani ya muda mfupi, na pia kuzingatia mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi unyevunyevu na maji zinashauriwa kutumika. 

Mamlaka husika zinashauriwa kuweka mipango tahadhari na kutoa elimu na ushauri kwa wakulima juu ya njia bora na namna ya kutumia kiwango kidogo cha mvua kinachotarajiwa Pamoja na matumizi mazuri ya chakula kilichopo.

"...Hali ya kupungua kwa magonjwa ya mifugo na mazao ya uvuvi kama samaki na mwani inatarajiwa. Mtiririko hafifu wa maji unatarajiwa kusababisha uzalishaji mdogo wa mazao ya samaki na mifugo. Aidha, kutokana na upungufu wa malisho na maji kuna uwezekano wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji kujitokeza. Wafugaji na wavuvi wanashauriwa watumie utabiri wa hali ya hewa na kufuata ushauri wa maafisa ugani."

Alibainisha kwa sekta ya usafirishaji inatarajiwa kunufaika hususan katika usafiri wa anga na nchi kavu, hivyo kushauriwa kutumia muda huu kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji hasa kwa ujenzi unaohusisha maeneo yanayoathiriwa na mafuriko. 

Msimu wa mvua za Oktoba – Disemba (Vuli) ni mahsusi katika maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ambayo ni nyanda za juu kaskazini-mashariki, pwani ya Kaskazini pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na Kaskazini mwa mikoa ya Kigoma na Morogoro. 


Sehemu ya wanahabari ikiwa ktika Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi (katikati) akizungumza alipokuwa akitoa kwa wanahabari utabiri wa mwelekeo wa msimu wa mvua kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2020 jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Huduma za Utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Hamza Kabelwa akifuatilia.

No comments:

Post a Comment