MSAJILI wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB), Mhandisi Patrick Barozi amewataka Watanzania na wahandisi wote waliopata fursa katika mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa, SGR kuwa wabunifu na kuongeza bidii ya kujifunza ili kuwezesha mradi huo kufanikiwa.
Akizungumza katika ziara yake ya kukagua mradi huo Mhandisi Barozi amesema mradi huo utakapokamilika utaachwa kwa Watanzania kuuendesha hivyo ni muhimu vijana waliopata fursa kujifunza kikamilifu ili kumudu kuuendesha kwa tija.
"Hakikisheni kila utaalam mnaupata ili taifa liweze kumudu kusimamia miradi yake na kubuni mingine itakayojengwa na kuendeshwa na Watanzania wazalendo," alisema Mhandisi Barozi akizungumza eneo la mradi huo.
Kwa upande wake, Naibu Meneja wa Ujenzi sehemu ya Morogoro-Dodoma-Makutupora km 422 Injinia Christopher Mangwera amesema hadi sasa takribani asilimia 42 ya mradi huo ujenzi wake umekamilika na wanajitahidi kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha haraka.
Amesema katika mradi huo asilimia 82 ni Watanzania na 18 ni wataalam kutoka nchi za nje hivyo wanauhakika wataumudu kuuendesha mradi huo utakapo kamilika.
Sehemu ya Morogoro-Dodoma-Makutupora km 422 ina stesheni 8 ambazo ni Morogoro, Mkata, Kilosa, Kidete, Gulwe, Igandu, Bahi na Makutupora.
No comments:
Post a Comment