MBIO ZA NMB BIMA MARATHON KUKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 100! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 7 September 2020

MBIO ZA NMB BIMA MARATHON KUKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 100!

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB - Filbert Mponzi akizungumza wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na Mbio za NMB Bima Marathon zitakazofanyika Jumamosi ijayo. Kushoto ni Mwakilishi wa waandaaji wa mbio hizo - Baraka Mtavangu na Mwakilishi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili – Dkt. Rehema Laiti.


BENKI
ya NMB inatarajia kukusanya zaidi ya Sh. milioni 100 kwa ajili ya matibabu ya watoto wenye saratani katika mbio za
NMB Bima Marathon zilizopangwa kufanyika Septemba 12 jijini Dar es Salaam.

Fedha hizo zinatarajia kupatikana kupitia kwenye ada ya ushiriki wa mashindano hayo kwa upande wa Kilometa 5 ambazo zitashirikisha wadau mbalimbali watakaojitokeza kushiriki katika mbio hizo zilizopangwa kuanzia jengo la Mlimani City.

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB - Filbert Mponzi alisema kuwa wanatarajia  kushirikisha jumla ya wanariadha 3,000 katika mbio hizo ambazo zimeandaliwa na kampuni ya The Africa Digital Banking Summit inayoongozwa na Baraka Mtavangu.


Hizi ndizo jezi zitakazo tumika wakati wa mashindano ya Mbio za NMB Bima Marathon.


Mponzi alisema kuwa, viingilio vyote vya mbio za kilometa 5 vitapelekwa kwenye hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya watoto hao. Alisema kuwa, mbio za kilometa 10 na 21 zitatumika zaidi kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa bima.

Tunajisikia fahari kudhamini mashindano haya kwa ajili ya kusaidia jamii. Tunaomba wadau washiriki ili kufanikisha lengo au kuzidi lengo hilo. Naomba pia nitoe rai kwa jamii nzima aidha kushiriki mbio hizi au kuwasajili ndugu na marafiki ili tuweze kuwagusa watoto wengi zaidi wenye saratani kupata matibabu hospitali ya Muhimbili,” alisema Mponzi.



Timu ya NMB ikiwa tayari kwaajili ya Mbio za NMB Bima Marathon.

Kwa upande wake Baraka Mtavangu ambaye ni Mratibu wa NMB Bima Marathon alisema sehemu za kujisajili ni Mlimani city karibu na KFC pamoja na hospitali ya muhimbili. Wale wote ambao tayari wameshajisali wanaweza kupata jezi zao hapo hapo Mlimani city karibia na KFC.

Mbali ya Benki ya NMB, wadhamini wengine ni kampuni za Bima za Sanlam, Strategies, Reliance na UAP.  Benki hiyo kama mdhamini mkuu imetoa Shilingi milioni 35 kwa ajili ya udhamini wa mashindano hayo.


No comments:

Post a Comment