MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa Kondoa waendelee kuwamini viongozi wanaoletwa na CCM ili walete maendeleo zaidi.
“Endeleeni kuiamini Serikali hii ili iendelee kuongoza, endeleeni kuwaamini viongozi wanaoletwa na CCM ili waendelee kuleta maendeleo zaidi. Ninaomba kura za Mheshimiwa Rais, wabunge na madiwani watarajiwa sababu ndiyo wataleta maendeleo katika maeneo yenu,” amesema.
Ametoa wito huo Septemba 13, 2020 wakati akizungumza na wananchi wa Kondoa Mjini na Vijijini waliofika kusikiliza sera za wagombea kwenye uwanja wa SabaSaba, wilayani Kondoa, mkoani Dodoma.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye alifika wilayani humo kumuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na wagombea ubunge wa Kondoa Mjini, Ally Makoa na Dkt. Ashatu Kijaji wa Kondoa Vijijini na wagombea udiwani wa CCM, amewataka wananchi hao watumie kipindi hiki kutafakari kwa kina na kuchagua viongozi wanaowafaa.
“Wananchi msiyumbe, tuna uchaguzi wa aina mbili. Uchaguzi wa kwanza ni kuchagua kiongozi anayeweza kuleta maendeleo na mwenye uwezo wa kuleta maendeleo na uchaguzi wa pili ni uchaguzi wa kishabiki wa kufuata upepo. Tutumie kipindi hiki kichagua viongozi wanaoweza kutusemea masuala la maendeleo,” amesema.
Akielezea miundombinu ya barabara, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya Tano imefanikiwa kuunganisha makao makuu ya mikoa kwa barabara za lami na hata katika baadhi ya wilaya huku akitolea mfano wa kutoka Babati hadi Kondoa, Kondoa hadi Chemba na Chemba hadi Dodoma.
“Sasa hivi tunataka kufungua barabara ya kutoka Babati hadi Orkesumet, na hii ya kutoka Handeni - Kiberashi – Kondoa – Singida iko kwenye Ilani yetu ya sasa ukurasa wa 73. Barabara hii ikitoka Handeni itapita Kilindi – Kiteto – Kondoa hadi Singida.”
Katika barabara za wilaya, Mheshimiwa Majaliwa amesema hizo zinashughulikiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ambao wamepatiwa sh. bilioni 1.840 na sh. bilioni 6.4 nyingine zilitolewa kwa ajili ya barabara za Kondoa vijijini kutoka makao makuu na kuunganisha kata hadi kata.
Kuhusu mikakati ya Serikali ya awamu ya tano kukuza uchumi, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuna watu wanabeza ujenzi wa reli na ununuzi wa ndege lakini wanasahau kuwa maendeleo hayaji bila maendeleo ya vitu. “Huwezi kupata maendeleo ya watu bila kuwa na maendeleo ya vitu,” amesisitiza.
Kwenye sekta ya kilimo, Mheshimiwa Majaliwa amesema wananchi wa Kondoa ni wakulima wazuri wa mazao mbalimbali na akawakumbusha wakazi hao jinsi ambavyo Serikali imeboresha upatikanaji wa mbolea na pembejeo za kilimo.
“Kilimo ndiyo kinasheheneza mkakati wetu wa uchumi wa viwanda. Na mpaka sasa, tumeshaanzisha viwanda 8,477 na hapa nasisitiza kuwa viwanda hivi na miradi ya kimkakati vimesaidia kuongeza ajira hapa nchini.”
“Lazina niwaeleze ukweli, mkikaa kusubiri ajira rasmi, nafasi ni chache mno. Ukitaka kazi huko Halmashauri au kwingineko, itabidi usubiri hadi walioko wastaafu. Ndiyo maana tumeanzisha miradi ya kimkakati ya reli ya Kisasa, mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere ili wananchi waweze kupata ajira huko.”
“Vijana wanaojiajiri kwenye ususi, kuchomelea nondo, wafanyabiashara ndogondogo wote hawa wana ajira. Ajira siyo siyo lazima iwe ile ya kushika kalamu ofisini,” amesisitiza.
No comments:
Post a Comment