WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Kassim Majaliwa amefuraishwa na mfumo maalum wa kuhakiki pembejeo za wakulima unaojulikana kama 'T-Hakiki' uliozinduliwa hivi karibuni na Shirika la Mawasiliani Tanzania (TTCL) kuwasaidia wakulima kutambua ubora wa pembejeo kabla ya kuzitumia.
Waziri Mkuu amevutiwa na mfumo huo alipotembelea Banda la TTCL kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa aliyoyafunga rasmi jana katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoa wa Simiyu. Alisema mfumo huo ni mzuri endapo utatumika vizuri kwa wakulima na unaweza kuwasaidia kupambana na pembejeo feki.
Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Waziri Kindamba alisema mfumo huo umetokana na ubunifu wa Shirika la Mawasiliani Tanzania (TTCL), Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Tropiki (TPRI/TAPHPA), wakilenga kumsaidia mkulima kutambua pembejeo feki, ikiwemo madawa, mbegu na mbolea wanazotumia.
Mkurugenzi Kindamba alisema ubunifu huo umeenda sambamba na malengo ya Rais Dk. John Pombe Magufuli katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo. "..Uuzaji wa pembejeo bandia za kilimo una athari kubwa kiuchumi na kijamii.
Kwa sasa huduma hii itamsaidia mkulima kufahamu matumizi sahihi ya pembejeo hizo kupitia simu ya mkononi. Alisema; "..T-Hakiki ni mfumo wa njia ya SMS ambapo mkulima atatakiwa kubofya *148*52# na kuingiza namba ya siri iliyopo kwenye vifungashio vya mbegu, mbolea au kwenye chupa za vifungashio vya mbegu, mbolea au kwenye chupa za viuatilifu ili kuthibitisha uhalisi wa pembejeo,"
Katika hatua nyingine TTCL imeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha watoa huduma za Mawasiliano nchini na vile vile TTCL imechukua ushindi wa tatu wa jumla katika maonesho ya NaneNane Kitaifa mwaka huu na kukabidhiwa vikombe vya ushindi huo jana kwenye sherehe za kuhitimisha maonesho hayo.
TTCL imekabidhiwa kikombe cha mshindi wa kwanza katika kipengele cha watoa huduma za Mawasiliano nchini jana na Waziri Mkuu Majaliwa huku kile cha ushindi wa tatu wa jumla kikikabidhiwa na Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga kwenye hafla za ufugaji wa maonesho hayo.
No comments:
Post a Comment