KLABU ya Simba imefanikiwa kutinga kibabe Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup baada ya kuifunga Azam FC kwa mabao 2-0.
Kwa matokeo hayo sasa Simba itakutana na Yanga SC katika Nusu Fainali ya Kombe hilo, maarufu kama Azam Sports Federation Cup baadaye mwezi huu. Simba imefanikiwa kuitoa Azam FC kwa kuichapa bila huruma mabao 2-0 katika mchezo wa mwisho wa Robo Fainali uliofanyika jana siku Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Mchezo mwingine nusu fainali wa kombe hilo utakuwa kati ya Sahare All Stars ya Tanga itakapokutana na Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi iliyoingia baada ya kuichapa Alliance FC ya Mwanza mabao 2-0.
Mshambuliaji hatari wa Simba, John Bocco (Nahodha) aliifunga Azam FC bao la kwanza dakika ya 39 kwa kichwa akimalizia pasi ya kiungo hatari, Francis Kahata kutoka upande wa kushoto wa uwanja. Baadaye Clatous Chama wa Simba alifunga hesabu kwa bao la pili dakika ya 56 akimalizia pasi ya beki Shomari Kapombe kutoka upande wa kulia wa uwanja.
Sahare All Stars ya Daraja la Kwanza imefanikiwa kutinga baada ya kuichapa Ndanda SC ya Mtwara kwa penalti 4-3, baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 za mchezo Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
Kikosi cha Simba; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’/Gardiel Michael dk88, Kennedy Juma/Erasto Nyoni dk46, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Gerson Fraga ‘Viera’, Clatous Chama, John Bocco, Luis Miquissone na Francs Kahata.
Wakati Azam; Benedict Haule, Nico Wadada, Salmin Hoza, Oscar Maasai, Abdallah Kheri, Mudathir Yahya/Bryson Raphael dk46, Bruce Kangwa/Iddi Kipagwile dk68, Frank Domayo, Richard Ella D’jodi, Never Tegere/Andrew Simchimba dk64 na Obrey Chirwa/Shaaban Iddi Chilunda dk76.
No comments:
Post a Comment