MAWASILIANO YAREJESHWA MTO RAU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 2 July 2020

MAWASILIANO YAREJESHWA MTO RAU

Muonekano wa Daraja la muda la Chuma la Mto Rau lililojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) baada ya daraja la awali kuharibiwa na mvua, daraja hilo ni kiunganishi kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ujenzi wa daraja jipya la kudumu unatarajia kuanza hivi karibuni.

Na Bebi Kapenya, Kilimanjaro
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), umeendelea kurejesha mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini yaliyoathiriwa na mvua zilizosababisha athari kubwa kwa watumiaji wa barabara pamoja na madaraja.
Wakala umejenga daraja la muda la Chuma la Mto Rau Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya daraja la awali linalounganisha Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Manispaa ya Moshi kuvunjika na kusababisha kukosekana kwa mawasiliano kwa wananchi wa maeneo hayo.
Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mhandisi Roy Johansen alisema baada ya kupata changamoto ya kuvunjika kwa daraja la mto Rau, Wakala ulichukua hatua za haraka za kurudisha mawasiliano kwa kutengeneza daraja la muda la Chuma lenye urefu wa mita 23 ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kwani eneo hilo linahudumia Kata 2 zenye jumla ya vijiji 9.
”Sisi kama Wakala tuliamua kutengeneza daraja la muda la Chuma kwa ajili ya wapita kwa miguu, pikipiki na bajaji ili kurudisha mawasiliano kwa wananchi kabla ya kutengeneza daraja jipya la kudumu, pia niwaombe wananchi wa maeneo haya wawe na uvumilivu kwani tutajitahidi kadri ya uwezo wetu ili mawasiliano ya awali yaweze kurudi”, alisema Meneja huyo.
Meneja alisema hatua itakayofuata ni kutengeneza daraja la kudumu ambapo tayari kwa kushirikiana na Ofisi ya Mratibu wa TARURA Mkoa wa Kilimanjaro jumla ya fedha kiasi cha shilingi milioni 650 zimeombwa TARURA Makao Makuu na tatizo hilo limeanza kushughulikiwa.
Aidha, Mhandisi Roy Johansen alisema, Wakala umetafuta ufumbuzi mwingine wa changamoto inayowakabili wananchi wa maeneo hayo kwa kuanza kutengeneza barabara ya Mandela Access iliyopo upande wa pili wa maeneo hayo yenye urefu wa Km 4 ambapo barabara hiyo itasaidia wananchi kusafirisha bidhaa zao kwa magari huku wakingojea kutengenezwa kwa daraja la kudumu.
Naye, Bw. Emmanuel Massawemkazi wa Kijiji cha Mamboleo ameishukuru Serikali kwa kutengeneza kivuko hiko cha muda na kusema kimewasaidia sana kutatua baadhi ya changamoto zilizokuwa zinawakabili na ameiomba Serikali kupitia TARURA kuwajengea daraja kubwa ili magari yaanze kupita kama hapo awali.
TARURA inaendelea kurejesha mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini baada ya mvua kunyesha kwa muda mrefu na kusababisha baadhi ya maeneo kutopitika.

No comments:

Post a Comment