WAZIRI HASUNGA AFUNGUA MAONESHO YA KILIMO BIASHARA 2020 TARI ILONGA, AGUSWA NA KASI YA TEKNOLOJIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 18 June 2020

WAZIRI HASUNGA AFUNGUA MAONESHO YA KILIMO BIASHARA 2020 TARI ILONGA, AGUSWA NA KASI YA TEKNOLOJIA



Waziri wa Kilimo  Japhet Hasunga, akisalimiana na  Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Taifa, Dk. Yohana Budeba, alipowasili kufungua Maonesho ya Kilimo Biashara  2020 yaliyofanyika kwenye Kijiji cha Majambaa Kata ya Msowero,  Kilosa mkoani Morogoro jana. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Dk. Geofrey Mkamilo.

Waziri wa Kilimo  Japhet Hasunga, akisalimiana na  Mkurugenzi wa  Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Ilonga, Dk.Joel Meliyo alipowasilli kufungua Maonesho hayo. Kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Kilimo MATI, Ilonga, Abdallah Gulana. 

 Waziri wa Kilimo  Japhet Hasunga, akitambulishwa watumishi, wadau na viongozi mbalimbali wanaofanya kazi kwa karibu na TARI Ilonga kabla ya kufungua maonesho hayo.
Mkurugenzi wa  Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Ilonga, Dk.Joel Meliyo, akiwasilisha taarifa ya tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo, mbele ya Waziri Hasunga kabla ya kufungua maonesho hayo.

Taarifa ikitolewa.
 Mkurugenzi wa  Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Ilonga, Dk.Joel Meliyo, akitoa maelezo kwa Waziri Hasunga, alipokuwa akitembelea shamba la ufuta katika maonesho hayo.
Waziri Hasunga, alikagua shamba la Mtama katika maonesho hayo.
Mashamba hayo pamoja na mengine hutumiwa na TARI kama mashamba darasa kwa wakulima na wanafunzi wa vyuo mbalimbali katika kupata ujuzi stahiki na teknolojia za kisasa kwa tija na mapinduzi ya kilimo.


Waziri Hasunga, alikagua mashamba darasa ya aina mbalimbali yanayosimamiwa na  TARI Ilonga katika maonesho hayo.




Wakulima wa Kijiji cha Msowero wakiangalia shamba darasa la kilimo cha mbaazi.





 Msimamizi wa Shamba la  Mbegu Msimba, kutoka  Kampuni ya Mbegu ya ASA, Mhandisi Johnson Ombeni, akimweleza Waziri Hasunga namna kampuni hiyo ilivyoboresha aina zake mbalimbali za mbegu.

 Wanafunzi wa Chuo cha Kilimo (MATI) Ilonga wakishiriki   maonesho hayo kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo. Chuo hicho maarufu kwa sasa kimezidi kujiimarisha katika teknolojia mbalimbali za kilimo na usindikaji kuendana na mahitaji ya soko. 

 Mkurugenzi wa  Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Ilonga, Dk.Joel Meliyo, akizungumza na wakulima.

 Wakulima wa Kijiji cha Msowero na maeneo mengine ya Wilaya ya Kilosa wakiendelea kupata elimu juu ya mapinduzi yenye tija kwa kilimo endelevu kupitia uwekezaji, ubunifu na biashara chini ya TARI Ilonga kwenye maonesho hayo.

 Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Dk. Geofrey Mkamilo, akizungumza mbele ya mamia ya wakulima (hawapo pichani) waliohudhuria maonesho hayo.


Mwonekano wa Shamba darasa la Mtama.
Mwonekano wa  Shamba darasa la alizeti.

 Mwonekano wa  Shamba darasa la mahindi.


 Afisa Mauzo wa Kampuni ya Mbegu ya SEED-CO, Athuman Mbonde, akimweleza Waziri Hasunga namna kampuni hiyo ilivyoboresha aina zake mbalimbali za mbegu.

 Mtafiti wa zao la Miwa TARI Kibaha Mkoa wa Pwani, Diana Nyanda, akitoa maelezo ya namna walivyoboresha mbegu mbalimbali za zao hilo mbele ya Waziri Hasunga.

 Mkuu wa Chuo cha Kilimo MATI, Ilonga, Abdallah Gulana, akimweleza Waziri Hasunga teknolojia mbalimbali za mafunzo kwa vitendo zinazofanyika chuoni hapo kupitia malighafi za kilimo kabla na baada ya usindikaji kufikia mahitaji ya soko. 

 Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Yohana Kastila akizungumza.

  Mkufunzi wa Chuo cha Kilimo MATI, Ilonga, Mariam Joseph (katikati), akimweleza Waziri Hasunga namna chuo hicho kilivyofanikiwa kuongeza thamani ya bidhaa zake mbalimbali zinazosindikwa kutokana na malighafi ya kilimo. 

Mwonekano wa Jengo la Utawala la Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI), Ilonga.

Na Godwin Myovela, Morogoro

KITUO cha Utafiti wa Kilimo TARI Ilonga kilichopo Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kimetakiwa kuweka mikakati ya kuhakikisha kinasambaza teknolojia  zilizogunduliwa na watafiti wake , sambamba na aina zote za mbegu bora kwa wakulima ili kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga wakati akifungua Maonesho ya Kilimo Biashara kwa mwaka huu yaliyofanyika kwenye Kijiji cha Majambaa, Kata ya Msowero wilayani Kilosa mkoani hapa jana.

"Kupitia maonesho haya wakulima wananufaika na teknolojia mbalimbali zinazozingatia kanuni za kilimo bora. Hivyo niitake Taasisi ya TARI kupitia  vituo vyake vyote kuhakikisha teknolojia hizi mnazoendelea kuzigundua kila kukicha zinawafikia walengwa," alisema Hasunga.

Aidha, Waziri wa Kilimo alikazia agizo lililotolewa na Naibu Waziri wake Omary Mgumba kupitia maonesho kama hayo yaliyofanyika mwaka jana,  kwa kukitaka kituo hicho cha utafiti kufanya maonesho kwenye maeneo ya wakulima ili kuwawezesha kujionea uhalisia na teknolojia za kilimo na usindikaji wa mazao yake.

Kauli mbiu ya maonesho ya kilimo biashara kwa mwaka huu ni 'Mapinduzi yenye tija kwa kilimo endelevu kupitia uwekezaji, ubunifu na biashara.

Hasunga akihutubia mamia ya wakulima kuzunguka wilaya ya Kilosa na maeneo jirani alisema takwimu za 2018 zinaonesha kilimo kinaajiri takribani asilimia 58 ya watanzania wote, huku kikichangia asilimia 28.2 ya pato lote la Taifa.

huku akisisitiza kati ya asilimia hizo, sekta ndogo ya mazao inachangia kwa asilimia 16.2 ya uchumi wa Taifa.

Sambamba na hilo alisema 2015 mpaka 2019 sekta ya kilimo imeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.2, huku sekta ndogo ya mazao ikikua kwa wastani wa asilinia 5.8.

" Kilimo chenye tija kitatuhakikishia uhakika wa chakula lakini pia lishe bora. Mpaka sasa Tanzania imeendelea kujitosheleza kwa chakula kwa zaidi ya asilimia 120." alisema Hasunga na kuongeza:

"Lakini ikumbukwe kwa sasa tuna ziada ya tani zaidi ya milioni 2.8 ambazo tunauza ndani na nje. Pia kilimo kinawezesha upatikanaji wa malighafi kwa zaidi ya asilimia 65 ya viwanda vyote vilivyopo nchini."

Akizungumzia namna ya kukabiliana na changamoto ya mitaji, Waziri aliwataka wakulima kuitumia Benki ya Kilimo (TADB), Mfuko wa Pembejeo na asilimia 10 ya fedha zinazotengwa na halmashauri kwa kukopa ili kuboresha kilimo

Alisema watanzania walio wengi bado wamejikita kwenye kilimo duni huku akiwasihi wakulima kuzingatia maelekezo ya watafiti hususan TARI Ilonga ili kuongeza tija, wingi wa mazao na fedha za kutosha

"Kituo hiki cha Tari Ilonga moja ya jukumu lake kubwa kwa sasa ni kuhaulisha teknolojia rafiki lengo hasa ni kumfanya mkulima aondokane na zana duni za kilimo ikiwemo matumizi ya majembe ya mkono na kilimo cha mazoea. Niwasihi wakulima huu ni wakati wa kutumia akili na teknolojia zaidi, na tukumbuke bila ya kukubali kubadilika na kuwa na mwamko hatuwezi kufikia hapo," alisema Hasunga

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi TARI Taifa, Dk.Yohana Budeba, alipongeza serikali kwa kuanzisha kituo hicho muhimu kwa ustawi wa kilimo nchini, huku akiwataka wakulima kuwatumia watafiti wa taasisi hiyo makini yenye vituo vyake takribani 17 kwa tija na ustawi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo nchini, Dk.Geofrey Mkamilo alisema kwa takribani miaka 77 mpaka sasa ya uwepo wa Kituo hicho kilichosheheni wasomi wabobevu kwenye masuala ya kilimo kimeendelea kuwa kinara katika  kuwezesha maboresho kadhaa kwenye sekta ya kilimo

Alisema pamoja na changamoto zilizopo, hususan fedha, uchakavu wa miundombinu, kukosa maabara na uhaba wa watumishi, lakini taasisi hiyo imeendelea kubuni na kuandika maandiko mbalimbali ya miradi kwa wadau wa maendeleo, ili kukidhi mahitaji muhimu ya lazima sambamba na kwenda na kasi za mabadiliko ya mara kwa mara ya kisayansi, kiutafiti na kiugunduzi katika kufikia malengo

"Natambua kilimo kina mambo makubwa matano ambayo ni chakula, biashara, ajira, viwanda na uchumi. Ili kuboresha kilimo chetu ni lazima tuweke mkazo na tuwekeze kwenye utafiti kwa maana ya kuwa na mbegu bora sanjari na zana bora za kilimo." alisema.

Naye mkuu wa kituo hicho Dk. Joel Meliyo alisema kituo cha TARI Ilonga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kimejikita katika kufanya tafiti na kuonesha teknolojia ya mazao yote kwenye eneo kilimo biashara

Meliyo aliwataja na kuwashukuru baadhi ya wadau wa kilimo wakiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kampuni ya Mbegu ya SEED-CO,  ASA, Magereza, vyuo vikuu na sekta nyingine binafsi kwa ushirikiano mkubwa na kituk hicho.

Alisema kituo hicho kina majukumu 5 ya kitaifa, ambayo ni utafiti wa mahindi, alizeti, mazao ha nafaka- yakiwemo mtama, ulezi na uwele, utafiti wa mazao jamii ya mikunde pamoja na utafiti wa teknolojia ya mazao baada ya mavuno.

Katika kutimiza majukumu hayo, baada ya utafiti kituo hicho kinatafuta namna ya kuweka teknolojia hiyo kwa lugha nyepesi ili kumiwezesha kila mkulima kuelewa.

Meliyo alisema pamoja na mambo mengine katika kufanikisha hilo, wameanzisha eneo la kilimo biashara ili kiwawezesha wakulima kutambua kilimo ni pamoja na chakula, fedha na kuimarisha uchumi kutokana na dhana yake kama chanzo cha malighafi.

"Teknolojia ya mbegu bora, agronomia (kwa maana ya nafasi kati ya mstari kwa mstari na mmea kwa mmea) teknolojia tunayotoa kwa sasa ni ya kumwezesha mkulima kuvuna kati ya  gunia 15 na 25 kwa ekari.. hii ina tija," alisema

Kupitia teknolojia zinazotolewa TARI Ilonga wakulima watapata chakula cha kutosha na viwanda vitapata malighafi sanjari na kusaidia kupunguza umaskini wa kipato.

"Nawasihi wananchi wote watumie muda wao mchache kuja kutazama na kujifunza. Kuna mbegu bora tofauti-tofauti zitakazo wawezesha kufanya uchaguzi pale msimu wa kilimo unapofika kwa tija na manufaa." alisema Meliyo

No comments:

Post a Comment