RC MAKONDA KUKAGUZI MIRADI YA MAENDELEO WILAYA YA KINONDONI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 18 June 2020

RC MAKONDA KUKAGUZI MIRADI YA MAENDELEO WILAYA YA KINONDONI

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo.

MKUU
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda anatarajiwa kufanya ziara ya siku mbili katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni yenye majimbo mawili, kuanzia Juni 20 hadi 21 mwaka huu itakayohusisha ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayoenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo amesema kuwa miradi hiyo ni ile iliyotekelezwa kwa kipindi cha Miaka mitano ya Uongozi wa Rais Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli, ambayo imetekelezwa kwa fedha ambazo ni vyanzo mbalimbli ikiwemo mapato ya ndani, Serikali Kuu na Wadau.
Amesema kwa kufanya hivyo ni kuonesha uzalendo hasa ikizingatiwa miradi hiyo imetekeleza kwa kiwango kilichokusudiwa na kukamilika kwa ubora na wakati uliopangwa.
“Miradi hii ambayo Manispaa imetekeleza nikutokana na dhamana ambayo CCM imetupatia na hivi sasa tunakwenda kukiabidhi ,nasio hii tu ambayo tumeitaja, Manispaa ya Kinondoni inamiradi mingi mikubwa ambayo imefanyika ila hii tumeichagua kama alama ya uwasilishwaji wa majukumu yetu,” amesema Mhe. Chongolo.
Ameitaja miradi ambayo itatembelewa kwa Jimbo la Kawe kuwa ni umaliziaji wa Hospitali ya Wilaya iliyopo Mabwepande, jengo la Mama na Mtoto RCH, nyumba ya watumishi wa Hospitali hiyo, Shule ya Sekondari ya wasichana Tumaini, Kiwanda cha kuchakata taka kilichopo Mabwepande, Kituo cha Afya Bunju, ujenzi wa mantaki matano ya maji yenye ujazo wa mita milioni saba pamoja na Zahanati ya Mikoroshini.
 Kwa upande wa Jimbo la Kinondoni Miradi itakayotembelewa ni ujenzi wa Kiwanja cha kisasa cha mpira kilichopo Mwenge, Kituo cha daladala Mwenge, Soko la Sinza Africasana, ujenzi wa Barabara ya Moroco mwenge yenye urefu wa kilomita 4.2, Hospitali ya Mwananyamala jengo la Mama na Mtoto,  Kituo cha Afya cha Kisasa Kigogo kilichojengwa kwa ghorofa tano, shule ya Sekondari Mzimuni kwa ngazi ya Ghorofa mbili pamoja na Soko la Kisasa Magomeni.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya Kinondoni amesema kuwa Manispaa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeweza kuboresha miundombinu ya sekta muhimu za Afya pembezoni mwa mji iliyopeleke wananchi kupata huduma za afya kwa urahisi, na ile ya elimu kwa wenye uhitaji  maalumu hali iliyofanikisha makundi haya maalumu kupata huduma stahiki.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni. 

No comments:

Post a Comment