NYUNGU YA MWAROBAINI HAINA MADHARA - PROF. MGAYA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 1 June 2020

NYUNGU YA MWAROBAINI HAINA MADHARA - PROF. MGAYA

Majani ya mwarobaini.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WANANCHI
wametakiwa kuendelea kujifukiza kwa kutumia miti na mimea ya asili ikiwemo mwarobaini katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Prof. Yunus Mgaya ametoa rai hiyo leo jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa mti wa mwarobaini hauna madhara yeyote bali ni mti wenye manufaa kwa tiba asili/mbadala ya magonjwa mbalimbali.

Prof. Mgaya amesema kumekuwepo na upotoshaji katika baadhi ya mitandao ya jamii ambayo ilimnukuu kwa kusema kwamba mti wa mwarobaini haufai kujifukiza kwa sababu una kemikali zenye sumu jambo ambalo si kweli.

“Mti wa mwarobaini unatibu magonjwa arobaini, majani yake yanatumika kutibu minyoo, magamba yanatumika kutibu homa na mafuta ya mti huu yanatumika kutengeneza sabuni kwa ajili ya ngozi, hivyo mti huu ni mzuri na una manufaa makubwa kwa jamii yetu,” Alisisitiza Prof. Mgaya

Aliongeza kuwa taasisi yake ilifanya utafiti kupitia maandiko mbalimbali na kupata njia mbili za kumpa nafuu mtu mwenye maradhi mbalimbali na kutaja njia hizo kuwa ni dawa lishe ambayo ina virutubishi vinavyoweza kujenga na kuimarisha kinga ya mwili ili mwili uweze kupambana na virusi na kumfanya mtu apone.

Ametaja njia ya pili kuwa ni kujifukiza kwa kutumia mimea au majani ya miti mbalimbali ambayo husaidia kufunguka kwa mishipa ya damu, kufungua kifua kinachobana pamoja na kuondoa uchovu na msongo wa mawazo.

“Mimea mingi ina mafuta tete 'essential oil' hivyo harufu mbalimbali za majani ya miti yanaingia haraka mwilini na hivyo kusaidia kufanya mwili kutulia, kifua kufunguka na lile joto linasaidia mishipa ya damu kufunguka na kufanya mfumo wa hewa kuwa mzuri kwenye mwili wa mtu na aina hii ya tiba imetumika miaka mingi barani afrika”.

Prof. Mgaya alisema kuwa katika utafiti huo NIMR ilipata idadi ndefu ya majani ambayo yanatumika na wananchi hususani Tanzania na makabila mbalimbali na hivyo walishauriana kuweka makundi matatu na endapo mtu atapata mmoja wa mmea mmoja wapo anaweza kujifukiza.

Alitaja kundi la kwanza ni mkaratusi, kivumbasi (kashwagala) na mchaichai, kundi la pili ni Karafuu(mbegu), tangawizi na limau (majani) na kundi la tatu alisema ni mwarobaini na mpera na kusisitiza kuwa wakati wa kujifukiza joto lisiwe kubwa na muda usizidi dakika kumi kwa watu wazima.

Hata hivyo alishauri vyombo vya habari ni vyema kufika kwenye taasisi yake kuweza kupata taarifa sahihi ambazo zitasaidia kutoa elimu kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment