Mkuu wa mkoa wa rukwa Mh. Joachim Wangabo. |
MKUU wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Nkasi kuwakamata watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa kula fedha zilizotokana na makusanyo ya Halmashauri na kujikopesha bila ya kuziwasilisha Benki na hatimae kuendelea kuibua hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini (CAG).
Mh. Wangabo ameipa TAKUKURU siku saba kuhakikisha watumishi hao waliokula kiasi cha Shilingi 27,674,300/= wanarudisha fedha hizo na endapo watashindwa kufanya hivyo basi wafikishwe mahakamnami haraka iwezekanavyo na kuonya kuwa wadaiwa wa makusanyo ya halmashauri wamekuwa kama ugonjwa wa saratani uliokosa dawa huku Mkurugenzi na Madiwani wanaosimamia halmashauri hiyo wakishindwa kuwawajibisha.
“Nimeambiwa hizi fedha zinawahusu watumishi wa halmashauri watatu, mmoja anadaiwa milioni nane, na wengine wawili milioni tisa tisa, imesemwa tu wachukuliwe hatua za kisheria, lakininhaikutoa muda, hadi lini hawa watu wawe wamechukuliwa hatua hizo za kisheria, n ahata kwenye maeneo mengi hakuna muda wa kushughulikia hizi hoja kwamba kufikia tarehe Fulani hii iwe imekwisha, hakuna, sasa hawa watumishi watatu, TAKUKURU mko hapa, kamata hawa watumishi watatu, shughulikeni nao haraka iwezekanavyo kuanzia leo,” Alisema.
Pia ameeleza kuwa kwa mujibu wa taarifa za CAG kwa mwaka wa fedha 2018/2019, mapato yaliyokusanywa bila ya uthibitisho wa kupelekwa benki ni shilingi 47,725,415/= huku shilingi 20,051,115 zikiwa zimerudishwa, lakini wadaiwa hao hawajirekebishi na matokeo yake taarifa za mfumo wa ukusanyaji wa mapato hadi tarehe 31, Mei, 2020 unaonesha makusanyo ambayo hayajapelekwa benki kufikia Shililingi 53,813,308.38/= na hivyo kuiamrisha TAKUKURU kuwashughulikia.
Mh. Wangabo ametoa maelekezo hayo leo 3.6.2020 katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kuhusu utekelezaji wa hoja za Ukaguzi na Mapendekezo ya CAG ambapo pia amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuhakikisha analipa madeni ya Madiwani ndani ya siku saba.
Mh. Wangabo amechukua hatua hizo ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Suleiman Jafo ambaye hivi karibuni katika ziara yake mjini Sumbawanga alimtaka Mkuu huyo wa Mkoa kutumia vyombo alivyonavyo kushughulika na wadaiwa wa fedha za makusanyo ambazo hazikuwasilishwa Benki.
No comments:
Post a Comment