WAZIRI MKUU APOKEA SH. MILIONI 500 KUKABILI CORONA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 14 April 2020

WAZIRI MKUU APOKEA SH. MILIONI 500 KUKABILI CORONA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya  Sh. 500,000,000/= kutoka kwa Kampuni ya Export Trading Group,  ukiwa ni mchango wa Kampuni hiyo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali za mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu- COVID - 19. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 14, 2020. Kutoka kushoto ni Afisa Uhusiano, Frank Mtui, Kiongozi wa Kampuni (Tanzania) Niladri Choudhury, Afisa Uhusiano, Fatma Ally.  ( Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na uongozi wa Kampuni ya Export Trading Group, baada ya kupokea hundi ya  Sh. 500,000,000/= ,  ikiwa ni mchango wa Kampuni hiyo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali za mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu- COVID - 19. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 14, 2020. Kutoka kushoto ni Afisa Uhusiano, Fatma Ally, Afisa Uhusiano, Frank Mtui na Kiongozi wa Kampuni (Tanzania) Niladri Choudhury.  ( Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea hundi ya mfano ya sh. milioni 500 kutoka kampuni ya Export Trading Group (ETG) zikiwa ni msaada kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaotokana na maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19) nchini.

Waziri Mkuu amepokea msaada huo leo (Jumanne, Aprili 14, 2020) ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma, kutoka kwa Mkurugenzi mkazi wa ETG, Bw. Nilladri Chowdhury aliyefuatana na maafisa uhusiano wa kampuni hiyo, Bw. Frank Mtui na Bi. Fatma Salum Ally.

Akizungumza mara baada ya kupokea kupokea msaada huo, Waziri Mkuu amewashukuru watendaji wa kampuni ya ETG kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya corona, ambapo hadi sasa kesi 49 zimeripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa huo nchini na wagonjwa saba wameshapona.

“Kwa niaba ya Rais wetu, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tunawashukuru kwa msaada huu ambao utaisadia Serikali kupunguza makali ya kuwahudumia wananchi wetu. Tunahitaji kuungwa mkono na wadau wengine kama ninyi,” amesema.

Waziri Mkuu amewataka wananchi wote wazidishe kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo hasa katika kipindi hiki. “Hatua tuliyofikia hivi sasa, maambukizi yameanza kuongezeka hasa kwa Dar es Salaam na Zanzibar. Tunajua kule kuna watu wengi na shughuli zote za kiuchumi zinaanzia pale, lakini hatuna budi kufuata masharti tuliyopewa ili kuzuia ugonjwa huu usisambae,” amesema.

“Serikali inatoa msisitizo kwa wananchi wazingatie maelekezo yanayotolewa kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka pamoja na kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.”

“Muhimu zaidi sote tuendelee kumuomba Mwenyezi Mkungu ili atupunguzie makali ya ugonjwa huu,” amesisitiza.

Mapema, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kampuni ya ETG, Bw. Mahesh Patel, Mkurugenzi Mkazi wa ETG, Bw. Nilladri Chowdhury alisema wameamua kuchangia ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika vita ya kupambana na ugonjwa huo.

“Mwenyekiti wetu amesafiri lakini kama kampuni, tumeamua kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu, na ametutuma tutoe mchango wa shilingi milioni 500. Tuna imani na tunaendelea kumuomba Mungu ili atuvushe katika kipindi hiki,” alisema.

Alisema kampuni yao inashughulika na masuala ya kilimo zikiwemo kusambaza pembejeo na kuongeza thamani mazao kupitia kampuni yao ya Kapunga iliyoko Mbeya, viwanda vitatu vya kubangua korosho vilivyoko Mtwara, Newala na Tunduru na viwanda vya kusindika mbegu za mafuta.

Pia wanatoa soko kwa wakulima kwa kununua mazao kama vile korosho, mbaazi, kokoa, mahindi, choroko na ufuta.

No comments:

Post a Comment