Kazi ya maandalizi ya ujenzi wa daraja ikiendelea katika eneo la Kiyegeya, mkoani Morogoro.
|
Kamwelwe amesema kuwa pamoja na mambo mengine, mpango kazi huo uwasilishwe ukiwa umehusisha shughuli zinazofanyika na zinazotarajiwa kufanyika pamoja na taarifa za kihasibu za ujenzi huo kuanzia ulipoanza hadi sasa ambapo ameeleza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kupata tathimini na kujua gharama halisi.
Waziri Kamwelwe ametoa agizo hilo akiwa mkoani Morogoro wakati akikagua maendeleo ya uboreshaji wa barabara ya mchepuko na maandalizi ya ujenzi wa daraja la Kiyegeya ambalo lilikatika hivi karibuni kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
“Hatuwezi kufanya kazi bila ya kuwa na mpango kazi wa maandishi, najua mwanzoni haikuwezekana kutoka na tukio hili kuwa la dharura, ila sasa namuagiza Mtendaji Mkuu Patrick Mfugale, kuhakikisha kuwa ifikapo Jumatatu ananiletea mpango kazi huu kwa ajili ya kupata rekodi sahihi za kihasibu na mpango wa maendeleo wa kazi", amesema Mhandisi Kamwelwe.
Aidha, Kamwelwe ameongeza kuwa daraja la kudumu katika eneo hilo linatarajiwa kujengwa licha ya kuwepo kwa changamoto ya uwepo wa maji mengi katika eneo hilo na kusababisha wakati mwingine magari kutumia njia moja badala ya mbili ikiwemo ile ya mchepuo ambayo ilijengwa kwa ajili ya kutatua kero ya foleni mahali hapo.
Kamwelwe, amefafanua kuwa suala la foleni katika eneo hilo limepungua kwani kwa sasa magari yanapita bila foleni tofauti na hali ilivyokuwa awali wakati wa tukio lilipotokea, hali iliyozua kero kubwa kwa wasafiri na wasafirishaji wa abiria na mizigo.
Kwa upande wake, msimamizi wa daraja hilo, Mhandisi Boniface Mkumbo, amesema kuwa yeye na timu yake wamejipanga vizuri kwani barabara ya mchepuo ambayo waliagizwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, kuijenga wakati alipofika katika eneo hilo kujionea hali halisi imekamilika na magari yanaendelea kupita.
Mhandisi Mkumbo, ameongeza kuwa kazi nyingine zinazofanyika kwa sasa ni kuanza ujenzi wa daraja lenyewe ambapo anasema kuwa ndani ya siku 14 daraja litakuwa limekamilika na itabakia kazi ya kurudishia lami.
Mnamo Tarehe 2 mwezi Machi, mwaka huu, daraja la Kiyegeya mkoani Morogoro liliharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na hivyo kusababisha adha kubwa kwa wasafiri na wasafirishaji kwa muda wa siku Tano kutokana na kukatika kwa daraja hilo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment