SHIRIKA LA IFC LATAKIWA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA UCHAMBUZI WA MAZINGIRA YA SEKTA BINAFSI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 11 February 2020

SHIRIKA LA IFC LATAKIWA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA UCHAMBUZI WA MAZINGIRA YA SEKTA BINAFSI


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto), akieleza umuhimu wa Serikali kushiriki kikamilifu katika uchambuzi wa mazingira ya Sekta binafsi kwa manufaa ya wananchi, wakati wa Mkutano na Meneja wa Shirika la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses, anaeziwakilisha nchi za Afrika Mashariki, Somalia na Malawi (kulia), jijini Dodoma.

Meneja wa Shirika la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses, anaeziwakilisha nchi za Afrika Mashariki, Somalia na Malawi (kulia), akieleza fursa zilizopo katika Shirika lake ikiwemo mikopo, wakati wa mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), akipeana mkono na Meneja wa Shirika la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses, anaeziwakilisha nchi za Afrika Mashariki, Somalia na Malawi (kulia), baada ya kumalizika kwa Mkutano ulioangazia Sekta Binafsi, jijini Dodoma.

Wajumbe wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Meneja wa Shirika la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses, anaeziwakilisha nchi za Afrika Mashariki, Somalia na Malawi (hawapo pichani), wakifuatilia kwa makini maelezo ya fursa zilizopo katika Shirika la IFC, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa nne kushoto), akipeana mkono na Meneja wa Shirika la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses, anaeziwakilisha nchi za Afrika Mashariki, Somalia na Malawi (wa tatu kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi wa wajumbe wa mkutano huo kutoka Tanzania na Shirika la IFC.

Na. Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma

SERIKALI ya Tanzania imeiomba Benki ya Dunia kupitia Shirika lake la Fedha (IFC), kufanya kazi ya uchambuzi wa kitaalamu wa mazingira ya Sekta Binafsi nchini kwa kushirikiana na Serikali ili kuweza kufanyia kazi kikamilifu taarifa za uchambuzi huo kwa manufaa ya Taifa.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipokutana na kufanya mazungumzo na Meneja wa Shirika la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses, anaeziwakilisha nchi za Afrika Mashariki, Somalia na Malawi.

Dkt. Mpango alisema kuwa msimamo wa Serikali ni kuwa kazi ya uchambuzi wa changamoto za mazingira ya Sekta Binafsi ifanyike kwa ushirikiano kati ya Serikali na IFC ili taarifa ya matokeo ya uchambuzi huo iweze kufanyiwa kazi kikamilifu badala ya taarifa hiyo kuachwa bila kufanyiwa kazi kutokana na ushirikishwaji hafifu kutoka katika taasisi hiyo.

“Tunataka kufanyia kazi taarifa ambayo tumeshiriki kuiandaa na tutakuwa tunatekeleza jambo letu sisi wenyewe”, alieleza Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango amelitaka Shirika hilo lijielekeze katika misaada ya kitaalam na fedha ili kukuza Sekta Binafsi kwa kuendana na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano hususan upande wa kilimo bila kuiacha nyuma Sekta ya viwanda kwa kuangalia namna wadau wa Sekta Binafsi wanavyoweza kupata utaalam kutoka IFC.

Aidha alibainisha kuwa Tanzania imewahi kufanya kazi za uchambuzi na Serikali ya Marekani mwaka 2011 wakati wa kupitia utekelezaji wa dira ya maendeleo na kuandaa mipango ya nchi, pia kuna mpango wa kuangalia mazingira ya biashara pamoja na jarida lenye hatua mbalimbali ambazo zilikubaliwa na Sekta Binafsi katika kukuza sekta hiyo na kutoa ajira kwa wananchi.

“Kazi yoyote lazima izingatie mipango ya Serikali katika kuendelea kuboresha mazingira ya kukua kwa Sekta Binafsi, kufanya biashara na kuwekeza”, aliongeza Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango alisema kuwa wamejadili pia kuhusu uwezekano wa IFC kutoa hati fungani ambayo kwa sasa inalipwa kwa dola iweze kutolewa kwa Shilingi ya Tanzania.  Hata hivyo alibainisha kuwa bado jambo hilo linahitaji uchambuzi wa kitaalamu kwa kuwa hati fungani haiwezi kutolewa bila nchi kufanya tathmini huru na makampuni ya kimataifa kuhusu nguvu yake ya kuweza kukopa kwenye masoko kama hayo.

Alisema kuwa hadi mwishoni mwa mwezi huu majibu yatatatolewa baada ya wataalamu kuchakata na kupata majibu ya kuendelea na jambo hilo au kulisitisha.

Kwa upande mwingine Serikali ya Tanzania imeiomba Benki ya Dunia kupitia Shirika hilo la IFC, kufuata Sheria za nchi inapotoa misaada ikiwemo ya Sekta Binafsi ili kujiridhisha iwapo misaada hiyo inamanufaa kwa taifa.

Aliyasema hayo baada ya kuwepo kwa misaada iliyotolewa kwa Sekta Binafsi na Shirika hilo ambayo haikufuata utaratibu wa utoaji misaada unaotumika nchini kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.

Dkt. Mpango alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria za nchi maombi yote ya misaada nchini ni lazima yapite kwenye kamati ya kitaalamu ya kuishauri Serikali kuhusu madeni na baadae kamati ya kitaifa ambayo itatoa ushauri kwa Waziri wa Fedha ili aweze kusema sawa, iwapo msaada huo unamanufaa kwa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses, alikubali kufanyia kazi ushauri wa Dkt. Mpango na pia alisema kuwa wamefanya mazungumzo na Serikali ili kusaidia kuboresha zaidi mazingira ya Sekta Binafsi ili iweze kuajiri watu wengi zaidi na kulipa kodi katika juhudi za kukuza uchumi wa nchi husika.

Shirika la IFC lipo chini ya Benki ya Dunia kwa ajili ya kusaidia nchi zinazoendelea kama Tanzania kuendeleza Sekta Binafsi pamoja na kutoa mikopo na misaada mbalimbali ambapo kwa sasa wameelekeza mikopo mingi kwenye Sekta ya Benki ambayo hutoa mikopo kwa kampuni ndogo na kubwa hapa nchini.

No comments:

Post a Comment