WANANCHI
wa Kijiji cha Mwangudo wilayani Meatu mkoani kinachopakana na Hifadhi
ya Jamii ya Makao pamoja na Pori la Akiba la Maswa wakisalimiana na
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliyefika kijijini hapo
kutangaza maamuzi yaliyotolewa na Rais Dk. John Pombe Magufuli kuhusiana
na matumizi ya mita 500 kando mwa hifadhi hiyo kutumika kwa shughuli
za malisho ya mifugo. Picha na Mpiga Picha
NA MWANDISHI WETU, SIMIYU
ZAIDI
ya ng’ombe 1, 400 wa wafugaji wa Wilaya za Itilima na Meatu mkoani
Simiyu wamekufa mikononi mwa Maafisa wa Pori la Akiba la Maswa baada ya
kushikiliwa hifadhini kwa kipindi cha miaka mitatu bila kupatiwa
huduma muhimu za chanjo, dawa, maji na malisho licha ya Mahakama kutoa
hukumu kwa wamiliki kurejeshewa mifugo yao.
Wafugaji
hao wamesema tangu mwaka 2017 ng’ombe 1, 484 walikamatwa kwa madai kuwa
walikuwa ndani ya pori hilo na kwamba licha Mahakama kuamuru
warudishiwe ng’ombe wao bado waliendelea kushikiliwa na kuendelea kufa
na kubaki 72 na kuwasababishia umasikini mkubwa.
Wafugaji
hao walifikisha kilio hicho kwenye mikutano wa hadhara ilioitishwa na
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliyefika katika vijiji vya
Laini A na Laini B wilayani Itilima, Mwangudo na Malwilo Wilayani Meatu
mkoani Simiyu ambapo walisema licha ya Mahakama kutoa uamuzi wafugaji
hao warejeshewe mifugo bado hawajarudishiwa mifugo yao hadi sasa na
kwamba inadaiwa kuwa mifugo hiyo imekufa.
Baadhi
ya Wamiliki wa mifugo hiyo ni walioshinda kesi kwa upande wa Itilima
ni Malimi Sendama, Ngasa Mbeho, Kongwa Tulutu na Maduhu Mbuli ambapo
walimkabidhi Waziri Mpina risiti mbalimbali zinazoonesha mifugo hiyo
kuuzwa kwa bei ya kutupa huku ngombe anayetakiwa kuuzwa laki 4 hadi 5
akiuzwa sh laki 1.
Wafugaji
wengine kwa upande wa Meatu waliodhulumiwa ng’ombe 345 ni Subi Maduhu,
Masunga Muhamali, Zengo Kusekelwa, Kija Badila ambapo mifugo yao
inadaiwa kufa huku mfugaji mwingine akidai ngombe wake 55 ambao Mahakama
iliamuru alipe faini ya shilingi milioni 1.4 ili arudishiwe mifugo yake
na alilipa faini hiyo lakini mifugo yake haijarudishwa hadi sasa.
Akiwasilisha
kilio kwa niaba ya wafugaji hao, Katibu wa Mbunge wa Itilima, Alex
Ngulukulu alisema wahifadhi hao walitoa maelezo kuwa ng’ombe 289
wamekufa jambo ambalo sio la kweli kwani askari wa hifadhi walikuwa
wanaendesha minada ya kuuza mifugo hiyo.
“Ng’ombe
walikuwa wanauzwa kwenye minada wakati kesi ikiendelea mahakamani na
tuna ushahidi wa kutosha wa risiti zote walizokuwa wanatoa kwa wanunuzi
wa mifugo hiyo” alisema Alex.
Diwani
wa Kata ya Tindabuligi, Tabu Maghembe alisema maelezo yaliyotolewa
kwamba mifugo hiyo imekufa hawakubaliani nayo kwani hakuna mlipuko
wowote wa magonjwa ulioripotiwa katika kipindi hicho na hivyo kumuomba Waziri
Mpina kufikisha kilio hicho cha wafugaji wa Itilima na Meatu kwa Rais
Dk. John Pombe Magufuli ili aingile kati waweze kupata haki yao kwani
kwa muda mrefu amekuwa akipigania haki za wanyonge.
Mbali
na malalamiko hayo pia wafugaji hao walilalamikia kitendo Maofisa wa
Pori la Akiba Maswa kutanua mpaka bila kuwashirikisha wananchi na hivyo
kuendelea kupunguza eneo la malisho na kusababisha usumbufu mkubwa kwa
wafugaji. Pia
wananchi wa Wilaya za Wilaya za Maswa na Meatu wamelalamikia mgogoro wa
mpaka katika Ziwa Kitangiri na kwamba wamekuwa wakizuiliwa kuvua na
kukamatwa kwamba wameingia wilaya ya Iramba Mkoa wa Singida.
Makamu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Juma Mpina amshukuru Rais
Dk. John Magufuli kwa kuruhusu matumizi ya mita 500 kutoka kwenye Pori
la Akiba la Maswa yatumike kwa shughuli za kulishia mifugo sambamba na
kuruhusu matumizi ya mita 60 kutoka kwenye mto kutumika kwa shughuli za
akunyesha maji mifugo yao jambo ambalo hapo kabla wananchi walikuwa
wakizuiliwa na kusababisha mifugo mingi kufa kwa kukosa maji na malisho.
Akizungumza
baada ya malalamiko hayo Waziri Mpina aliwaagiza Wakuu wa Wilaya za
Itilima na Meatu kuitisha kikao cha pamoja kitakacho mhusisha Mhifadhi
Mkuu wa Pori la Maswa, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania na
Mwanasheria wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wafugaji wanaolalamikia
kudhulumiwa mifugo yao na kupitia vielelezo vyote vilivyotumika
kukamata, kutunza na kuuza mifugo pamoja na kupitia hukumu ya Mahakama
ili haki iweze kutendeka .
Pia
ameagiza Kamishna wa Ardhi, Mkurugenzi wa Uvuvi Tanzania, Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Meatu na Mkurugenzi wa Iramba ili kupitia upya mipaka
hiyo na kumaliza kabisa mgogoro huo kuhusu uvuvi katika Ziwa Kitangiri
Kuhusu
suala la kutanua mpaka kiholela, Waziri Mpina ameagiza timu ya
Wataalamu kutoka Wizara nane kupita kwenye maeneo yanayolalamikiwa na
kupima upya mipaka hiyo kwa uwazi na kwamba wananchi watashiriki katika
zoezi hilo. Aidha
kuhusu upungufu wa maeneo ya malisho vijiji saba vinavyounda WMA ya
Makao, Waziri Mpina aliagiza wafanye tathmini ya mahitaji ya ardhi ya
wananchi kwa sasa na kuandaa GMP itakayoruhusu baadhi ya maeneo kutumika
kwa ajili ya kulishia mifugo.
Hivyo
Waziri Mpina ameagiza wafugaji wote mkoani Simiyu walioshinda kesi
mahakamani na kutakiwa kurejeshewa mifugo yao kuwasilisha vielelezo vya
hukumu za kesi hizo kwenye ofisi za Wakuu wa Wilaya za Itilima na Meatu
ili haki iweze kutendeka. Mbali
na hayo Serikali imetenga zaidi ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya
kuangamiza wadudu aina ya mbung’o katika vijiji vyote vinavyopakana na
WMA Makao na maeneo mengine nchini ili kutokomeza kabisa mdudu huyo
hatari kwa mifugo.
No comments:
Post a Comment