MWAKALINGA AKABIDHI VIFAA VYA MAFUNZO CHUO CHA UJENZI MOROGORO. - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 18 February 2020

MWAKALINGA AKABIDHI VIFAA VYA MAFUNZO CHUO CHA UJENZI MOROGORO.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga, akizungumza na wanafunzi pamoja na watumishi wa Chuo cha Ujenzi Morogoro, alipofika chuoni hapo kukabidhi vifaa vya kufundishia wanafunzi ikiwemo mtambo mmoja (Grader) na Kompyuta 20.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga (wa kwaza kulia) akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa kukabidhi vifaa vya kufundishia wanafunzi wa Chuo cha Ujenzi Morogoro. Vifaa hivyo ni mtambo mmoja (Grader) na kompyuta 2o.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga, akionesha Kompyuta alizozikabidhi kwa uongozi wa Chuo cha Ujenzi Morogoro, kwa ajili ya kufundishia wanafunzi wanaosoma katika chuo hicho. Katibu Mkuu alikabidhi Kompyuta 20 na mtambo mmoja (Grader).

Wanafunzi wa Chuo cha Ujenzi Morogoro wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga (hayupo pichani), wakati akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa vya kufundishia wanafunzi hao ikiwemo mtambo mmoja (Grader) na Kompyuta 20, chuoni hapo.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, amekabidhi mtambo mmoja (Grader) na Komyuta 20 kwa Uongozi wa Chuo cha Ujenzi Morogoro na kutoa wito kwa wazazi, walezi, wafadhili na waajiri wote kuwapeleka vijana na watumishi wa jinsia zote  kupata mafunzo ya ufundi stadi ili kuweka uwiano mzuri kati yao.

Wito huo ameutoa mkoani Morogoro akiwa kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo ambapo pamoja na mambo mengine Katibu Mkuu huyo amesema kuwa hafurahishwi na kuwepo kwa idadi ndogo ya wanawake katika baadhi ya kozi, Chuoni hapo.

"Nimesikitika kupata taarifa kutoka kwa Mkuu wa Chuo kuwa kozi nyingi zina idadi kubwa ya wanaume kuliko wanawake na nyingine zina wanaume pekee, elimu ya ufundi stadi ni kwa wote, shime jinsia zote kushiriki kupata mafunzo haya", amesema Mwakalinga.

Katibu Mkuu Mwakalinga, amefafanua kuwa utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana utatoa mchango mkubwa katika azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ya kujenga uchumi wa kati na wa viwanda ambapo fani za ujenzi ni muhimu katika kufikia azma hiyo.

Aidha, Mwakalinga ameupongeza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kwa kukubali kutoa mtambo mmoja (Grader) na Wizara kutoa kompyuta 20 ili vitumike kufundishia wanafunzi ambapo amesema kuwa vifaa hivyo vitakuwa chachu ya utoaji mafunzo hapo chuoni.

"Naamini sasa kuja kwa vifaa hivi kutarahisisha na kuhamasisha mafunzo kwa vitendo, nawasihi mtumie vifaa hivi kwa malengo yaliyowekwa pamoja na kuvitunza vizuri", amesisitiza Katibu Mkuu Mwakalinga.

Sambamba na hilo Katibu Mkuu Mwakalinga amesema kuwa Wizara ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha Taasisi ya Teknolojia yaUjenzi kwa kuunganisha Chuo cha Ujenzi Morogoro na Chuo cha Teknolojia Stahiki ya Nguvukazi kilichopo Mbeya ambapo amefafanua kuwa lengo la kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ni kuboresha mafunzo yanayotolewa na vyuo hivyo viwili.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Morogoro, Melkizedeck Mlyapatali amesema kuwa chuo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa watumishi wakiwemo wahandisi wa fani mbalimbali, wakufunzi, wahasibu na wafanyakazi wengine kutokana na wafanyakazi wengi kustaafu kwa mujibu wa sharia na wengine kufariki dunia.

Chuo kina jumla ya wanafunzi 403 na kinaendesha mafunzo ya ufundi stadi na masomo ya kawaida kwa lengo la kuwezesha wahitimu kuwa mahiri katika Nyanja za ujenzi.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, 
Wizara ya Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment