BENKI ya NMB ilisema hapa mwishoni mwa juma kuwa itaongeza maradufu uwekezaji wake kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ya Serikali nia ikiwa ni kushiriki kikamilifu kwenye juhudi za Serikali za kuleta maendeleo nchini.
Hayo yalisemwa hapa mwishoni mwa juma na Kaimu Mkurugenzi wa NMB Bank – Ruth Zaipuna wakati menejimenti ya Benki na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya NMB – Prof Joseph Semboja walipokutana na kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC).
Katika wasilisho lake kwa kamati, Bi Zaipuna alisema kuwa mpaka sasa, Benki ya NMB imeshiriki kikamilifu katika kusaidia miradi mikubwa ya kimkakati ya Serikali kama ujenzi wa reli ya kisasa SGR (Standard Gauge Railway), Mradi Mkubwa wa Umeme wa Gesi wa Kinyerezi na miradi ya umeme vijijini iliyo chini ya mamlaka ya umeme vijijini REA.
“Tumeshatoa garantii ya shilingi bilioni 140 kwaajili ya mradi wa SGR na tutaendelea kutoa mchango wetu kwenye miradi mkakati ya Serikali yote ikiwa ni kuharakisha maendeleo ya watanzania.” Alisema Bi Ruth
Alisema kuwa, NMB imesimamia miamala ya barua za mikopo (Letter of Credit LC) yenye thamani ya shilingi bilioni 550 kwa mradi wa bomba la maji la Tabora, Igunga na Nzega, bilioni 35 pia kwaajili ya maboresho ya miradi ya maji ya DAWASA.
Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi Dar es Salaam, Ujenzi wa Barabara vijijini ulio chini ya TARURA, Bohari kuu ya Madawa na Mamlaka ya Bandari ni baadhi ya miradi mikubwa ya kimkakati ya Serikali ambayo imepata uwezeshaji wa aina mbalimbali wenye thamani ya mabilioni ya shilingi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) – Dr Raphael Chegeni aliisifu Benki ya NMB kwa uharaka wake kusaidia miradi mikubwa ya Serikali.
“Kama Bunge, tunafurahishwa sana na uamuzi wenu wa kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ya Serikali na tunaimani kubwa na menejimenti ya Benki hii na tunaamini mbele yenu ni nzuri Zaidi katika sekta ya mabenki.” Alisema Mh Chegeni.
Kuhusu uimara wa Benki, Bi Zaipuna alisema kuwa Benki ya NMB ni imara akiwahakikishia wabunge kuwa hesabu za mwaka 2019 ambazo zitatolewa mwisho wa mwezi huu, zitakuwa bora Zaidi kuliko mwaka 2018.
“Ikiwa ni taasisi iliyooroidheshwa kwenye soko la hisa, kwa sasa tupo kwenye kipindi cha kufunga mahesabu yam waka ambapo hatutakiwi kusema namba za mwaka 2019 mpaka mwisho wa mwezi huu ambapo tunaruhusiwa kisheria kutangaza, lakini tuna Imani kuwa zitakuwa bora kuliko mwaka 2018,” alisema Bi Ruth.
Benki ya NMB ilipata faida baada ya kodi ya shilingi Bilioni 156, Bilioni 150, Bilioni 154, Bilioni 93, Bilioni 98 kwa mwaka 2014, 2015,2016,2017 na 2018.
No comments:
Post a Comment