JUKUMU LA KUDUMISHA AMANI NA USALAMA WA NCHI NI LA WANANCHI WOTE-DK SHEIN - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 11 January 2020

JUKUMU LA KUDUMISHA AMANI NA USALAMA WA NCHI NI LA WANANCHI WOTE-DK SHEIN

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema jukumu la kudumisha amani na usalama wa nchi ni la wananchi wote na sio la vyombo vya ulinzi na Usalama pekee.

Dk. Shein amesema hayo viwanja vya Mnazimmoja mjini hapa, baada ya kupokea matembezi ‘amsha amsha’, yaliyowashirikisha Makamanda na wapiganaji wa vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na Idara maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Amesema kila mwananchi ana jukumu la kudumisha amani iliopo nchini pamoja na kulinda na kuyaenzi kikamilifu Mapinduzi  ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Alisema hatua ya wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama ya kuanzisha  aina hiyo ya matembezi, inafaa kupongezwa kwani inafanikisha dhamira ya kuwajengea ari wapinaji pamoja na kuwajengea matumaini wananchi ya kuendelea kuiamini Serikali yao.

Alisema dhana ya kudumisha usalama wa nchi inatokana na Sera ya chama cha Afro Shirazi Party (ASP) iliyowekwa baada ya Mapinduzi ya 1964, na kusema dhana hiyo ni endelevu na haitokuwa na  mbadala. Dk. Shein alisema baada ya Mapinduzi ya 1964, Zanzibar ilianzisha Jeshi la Ukombozi (JLU) na baada ya Muungano wa Tanzania, Jeshi la wananchi wa Tanzania liliundwa, lengo kuu likiwa ni kudumisha ulinzi na usalama  ndani na nje ya mipaka yake.

Alisema Wakoloni mbali na kutunza usalama katika kipindi cha Utawala wao, uamuzi wao haukuwa wa kisera, wakati ambapo hivi sasa kila kikosi kina sheria na kuongozwa kwa taratibu, hali inayovifanya vikosi hivyo kuwa na nidhamu ya hali ya juu.

Alisema Serikali zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ziko salama, zikitoa fursa kwa watu mbali mbali duniani kuja nchini na kufanya yale wanayoyapenda, ikiwemo utalii, ‘honey moon’ na mapumziko.

Aidha, alisema utulivu na usalama wa kutosha uliopo hapa nchini, imekuwa kivutio kikubwa cha kuvutia watalii kuja kwa wingi nchini, na kusema kumekuwepo ongezeko la ujio wao kutoka 520,000 mwaka uliopita (2017/2018)  hadi kufikia 540,000 mwaka huu.  

Alieleza kuwa Utalii umekuwa na tija kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi  pamoja na kuleta ustawi bora wa wananchi wa Zanzibar. Katika hatua nyengine, Rais Dk. Shein alikemea tabia ya baadhi ya watu ya kujifanya wababe na kuidharau Serikali  na kusema kila jambo lina mipaka yake, akibainisha usawa uliopo kwa kila mwananchi mbele ya sheria.

Alisema Serikali zote mbili za SMT na SMZ zinaendeshwa kwa misingi ya sheria, chini ya usimamizi wa vyombo vilivyowekwa ambavyo hufanyakazi kwa misingi ya katiba na sheria. Aliwataka wale wote waliojiandaa kufanya vituko kwa kisingizo cha uchaguzi mkuu mwaka huu kuacha mara moja na kubainisha kuwa Zanzibar ni nchi ya Mapinduzi iliopinduliwa ili wananchi waweze kuishi kwa amani na usalama.

Alisema siasa isiwe sababu ya watu kufanya fujo na kusema uchaguzi unaendeshwa kwa misingi ya sheria, akibainisha azma ya Serikali ya kuwashughulikiya wale wote watakaojihusisha na uvunjifu wa amani. Alieleza kuwa vyombo vya ulinzi viko makini na vinajuwa wajibu wao na kufafanua kuwa hakutakuwepo na mtu atakaeonewa katika ushughulikiaji wa jambo hilo.

Aidha, Dk. Shein aliwakumbusha wapiganaji hao kuwa suala la ulinzi na kuitetea nchi halina mbadala, akiahidi Serikali zote mbili kuendelea kubaki salama kwa vile zimejidhatiti kulinda mipaka yake ardhini na baharini.

Alieleza kuwa wapiganaji hao wana wajibu wa kulinda nchi na kusema yeyote atakaekuja kwa dhamira ya kuchochea machafuko, taratibu za kisheria zitachukuliwa. Aliwataka wananchi wote kuishi na kuendelea kufanya shughuli zao bila khofu, kwani vyombo vyao viko imara kuwalinda nyakati zote.  

Nae, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za mitaa na Idara maalum za SMZ, Haji Omar Kheir aliwashukuru makamanda na wapiganaji wa Vikosi hivyo  kwa kushiriki vyema na kufanikisha matembezi hayo.

Aidha, alisema zoezi la namna hiyo ambalo pia limefanyika kisiwani Pemba, litaendelea kufanyika mara kwa mara ili kuwaweka sawa  wapiganaji.

Mapema, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Halmashauri ya sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa, Brigedia Jenerali Fadhil Omar Nondo, alisema lengo la ‘amsha amsha’ ni kujenga ari na uwezo miongoni mwa vikosi hivyo pamoja na kuwajengea wananchi matumaini juu ya kuwepo kwa vikosi vyao makini.

Alisema zoezi hilo lililoratibiwa na wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama hufanyika kila mwaka, ambapo katika miaka iliyopita lilifanyika kwa mfumo wa ‘root march’ na kufanyiwa mabadiliko mwaka huu, na kuwa katika mfumo wa ‘amsha amsha’. Alisema zoezi hilo limewasharikisha wapiganaji kutoka JWTZ, Polisi, Uhamiaji, KMKM, Mafunzo, JKU,KVZ na Zimamoto linalenga kuyaenzi, kuyalinda na kuyatetea Mapinduzi ya 1964.

Aidha, alisema zoezi hilo lililoongozwa na kikundi cha JWTZ chini ya Kamanda Kanali Said Khamis lilitokana na njia kuu tatu tofauti (roots) zilizoanzia Mtoni na kuwakutanisha wapiganaji wote eneo la Ziwani, na kuendelea na matembezi hayo hadi Uwanja wa Mnazi mmoja, yakifuatiwa na vyombo mbali mbali vya usafiri pamoja na vifaa vinavyotumiwa na wapiganaji hao.

No comments:

Post a Comment