Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameiomba Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) kusaidia upatikanaji wa fedha kwa njia ya mikopo nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ikiwemo reli ya kisasa, nishati na kilimo.
Dkt. Mpango ametoa maombi hayo Jijini Dodoma, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa JICA, Dkt. Nobuko Kayashima, ambapo wawili hao wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa miradi inayokusudiwa kufadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika hilo.
Amesema kuwa hivi sasa Serikali imeelekeza nguvu na fedha zake za ndani kujenga Reli kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji ya Mto Rufiji mkoani Pwani (Nyerere Hydral Power Plant), na kwamba miradi inahitaji fedha nyingi ambazo anaamini Japan inaweza kusaidia upatikanaji wake.
“Tumeanza kutekeleza miradi hii kwa kutumia fedha zetu za ndani na tunaiomba Serikali ya Japan kuzishawishi taasisi zake za fedha kwa kushirikiana na taasisi nyingine kutupatia mikopo yenye masharti nafuu ili tuweze kukamilisha miradi hiyo muhimu kwa Taifa” alisema Dkt. Mpango.
Alifafanua kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza shughuli za kiuchumi na kibiashara hapa nchini pamoja na nchi jirani ambazo hazijapakana na Bahari huku nishati ya umeme ikitarajiwa kuboresha upatikanaji wa umeme kwa ajili ya kuendesha reli hiyo pamoja viwanda.
Aidha, Dkt. Mpango amemwomba kiongozi huyo wa JICA kusaidia Wizara na Serikali kwa ujumla kuendeleza rasilimali watu ama nguvu kazi kwa kuwapatia fursa ya masomo nchini Japan wataalam kutoka Wizara yake na maeneo mengine serikalini ili kuongeza ubobezi wa wataalam hao katika sekta ya uchumi, fedha, pamoja na tiba hususan matibabu ya moyo na figo.
“Pia ninaliomba Shirika lako lisaidie kuboresha miundombinu ya barabara za kuzunguka Jiji la Dodoma kutokana na mahitaji makubwa baada ya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi, pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nsalato-Dodoma” aliongeza Dkt Mpango.
Alisema kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa-Msalato unahitaji kujengwa njia ya kuruka na kutua ndege pamoja na ujenzi wa majengo ya abiria.
“ Pia nimewaomba wenzetu ambao wanauzoefu mkubwa watusaidie katika kilimo cha mpunga na nimetoa mfano wa Bonde la Ruvu ambalo ni kubwa na lina fursa ya kuzalisha mchele wa kutosheleza mahitaji ya ndani na nje na tukichagua eneo moja na kulitumia vizuri tutamaliza mahitaji ya mchele katika Taifa letu” alisisitiza Dkt. Mpango.
Akijibu maombi ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Makamu huyo wa Rais wa JICA, Dkt. Nobuko Kayashima, alikubali maombi ya kusaidia kuendeleza rasilimali watu ambapo kwa kuanzia Shirika hilo limeahidi kutoa nafasi ya watumishi 15 kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Sekta nyingine kupata ufadhili wa masomo nchini Japan.
Amesema Serikali ya Japan kupitia Shirika lake litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi ambapo miradi mipya inayokusudiwa kufadhiliwa na Shirika lake ni Mradi wa Upanuzi wa Bandari ya Kigoma, Ujenzi wa Barabara ya Arusha-Holili na Mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Zanzibar.
Kuhusu uendelezaji wa kilimo, Dkt. Kayashima ameahidi kuwa Shirika lake litaendelea kujihusisha na kuendeleza zao la mpunga hapa nchini ili kuwasaidia wakulima kujikimu kimaisha pamoja na kusaidia nchi ijitosheleze kwa chakula.
No comments:
Post a Comment