WAZIRI KAMWELWE AITAKA TANROADS KUTOYUMBISHWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 13 December 2019

WAZIRI KAMWELWE AITAKA TANROADS KUTOYUMBISHWA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), (hawapo pichani), wakati wa ufunguzi wa baraza hilo la 13 lililofanyika mkoani Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), (hawapo pichani), wakati wa ufunguzi wa baraza hilo la 13 lililofanyika mkoani Kagera.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, ameutaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kusimamia kwa uadilifu pasipo kuyumbishwa taratibu za manunuzi ya umma na wala kutoruhusu kuingiliwa na watu wenye maslahi binafsi.


Aidha, ameutaka Wakala huo kutafuta mbinu na mkakati mpya wa kukabiliana na vitendo vya utovu wa nidhamu na rushwa unaofanywa na baadhi ya watumishi wa mizani kwani unaharibu taswira na uaminifu wa Wakala huo.

Waziri Kamwelwe ametoa kauli hiyo jana mkoani Kagera wakati akifungua mkutano wa kumi na tatu (13) wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS nchi nzima ambapo pamoja na mambo mengine amefurahishwa sana na utekelezaji wa maagizo yake katika kikao kilichopita ambayo ni kielelezo cha usikivu, ukomavu na utii wa hali ya juu kwa Serikali.

"TANROADS msiyumbishwe katika taratibu za manunuzi na mtafute mbinu mpya ya kukabiliana na rushwa kwenye masuala ya ujenzi na mizani ili isiwaaharibie sifa yenu mliyonayo", amesema Waziri Kamwelwe.

Mhandisi Kamwelwe ameusisitiza Wakala kuendelea kuwajengea uwezo watumishi kwa kuwaongezea weledi  na kuwapa vitendea kazi na vifaa hasa Kitengo cha Usimamizi wa Miradi (TECU) ili kiweze kusimamia miradi mikubwa zaidi nchini. 

"Naendelea kuwasihi na kuwatia moyo kuendelea kuchapa kazi kwa kutanguliza mbele maslahi mapana na Taifa na tunajua uwepo wa upungufu wa watumishi, vitendea kazi pamoja na ofisi kwa baadhi ya mikoa, jambo hilo lisiwavunje moyo na liwe chachu na hamasa ya kuwajibika, nasi tutaendelea kutafuta na kuweka mikakati mbalimbali ya kutatua changamoto hizo kwa kuzingatia vipaumbele ili tuweze kuhakikisha kuwa hakuna jambo lolote linaloweza kukwamisha utekelezaji wa majukumu yenu", amesisitiza Mhandisi Kamwelwe.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, amesema kuwa Wakala unaendelea kutekeleza na kuhakikisha kuwa miradi mbalimbali ya kimkakati na ile ya maendeleo inakamilika kwa wakati na viwango ili iweze kuchochea kasi ya maendeleo ya nchi yetu.

Ameongeza kuwa kasi ya usimamizi na ukamilishaji wa miradi mikubwa kwa wakati itaenda sambamba na thamani ya fedha (Value for money katika miradi yote nchini na hivyo kuifanya TANROADS kuendelea kuwa injini ya uchumi wa Taifa letu katika ujenzi wa uchumi wa kati.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, ameipongeza TANROADS kwa kwa juhudi, maarifa na utendaji kazi kwa weledi ambao unaweka mbele maslahi mapana ya nchi yetu.

"Sisi sote hapa ni mashahidi wa kuona jinsi Serikali inavyoamua miradi mingi mikubwa isimamiwe na TANROADS na katika hili hamjatuangusha", amesema Mkuu wa Mkoa. 

Waziri Mhandisi Kamwelwe yupo mkoani Kagera kwa ziara ya siku mbili ambapo atakagua pia miradi ya barabara, madaraja, bandari inayoendelea kutekelezwa na Wizara yake.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment