UHUISHAJI TAKWIMU ZA WAKIMBIZI...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 3 December 2019

UHUISHAJI TAKWIMU ZA WAKIMBIZI...!

Wakimbizi wakiwa nchini Tanzania
Na Veronica Mwafisi, Dar es Salaam
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, kesho Desemba 3, mwaka huu, itafanya uzinduzi wa kuhuisha takwimu za wakimbizi waishio jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo utafanyika katika Ukumbi wa Polisi Officer’s Mess, Oysterbay, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Huduma kwa Wakimbizi katika Wizara hiyo imefafanua kuwa, uhakiki huo utafanywa na idara hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
“Uhuishaji takwimu utahusisha wakimbizi wote waishio Dar es Salaam wenye nyaraka, walioruhusiwa kuishi nje ya kambi za wakimbizi na maeneo mengine kuanzia saa 2 asubuhi,” ilifafanua taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya uzinduzi uhuishaji takwimu utafanyika katika Ofisi za Shirika la Relief of Development Society (REDOSO). Ofisi hizo zipo Kinondoni, Biafra ambapo wakazi, waombaji hifadhi wote pamoja na familia zao, wanapaswa kufika ili kuhuisha takwimu zao bila kukosa.
Mkimbizi yeyote ambaye hatajitokeza wakati wote wa uhuishaji takwimu taarifa zake hazitahuishwa na usajili wake utasitishwa. Wakimbizi hao wametakiwa kufika na nyaraka za utambulisho zikiwemo barua ya uthibitisho wa mkimbizi, usajili, kibali cha kuishi nje ya kambi, vyeti vya kuzaliwa.
Wakimbizi wakiwa nchini Tanzania
Nyaraka nyingine ni vyeti vya ndoa, hati ya kusafiria, vitambulisho vya kazi, shule, chuo na nyaraka nyingine yoyote inayomtambulisha mkimbizi ambayo inatambulika kisheria.
“Shughuli zote zinazohusiana na uhakiki wa taarifa za mkimbizi na waomba hifadhi zinatolewa bure.

“Uhuishaji huu hautahusisha wakimbizi wa mwaka 1972 wanaotoka makazi ya Ulyankulu, Katumba, Mishano na waishio vijijini mkoani Kigoma,” ilieleza taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment