DC CHONGOLO AZINDUA MAONESHO YA BIDHAA ZA NGOZI, AWEKA MKAKATI WA SOKO LA UHAKIKA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 13 December 2019

DC CHONGOLO AZINDUA MAONESHO YA BIDHAA ZA NGOZI, AWEKA MKAKATI WA SOKO LA UHAKIKA

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo akiangalia viatu vya ngozi. Kulia ni Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Patricia Henjewele.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni , Mhe. Daniel Chongolo akipewa maelezo na mjasiriamali anayezalisha viatu vya ngozi. Kulia ni Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Dk. Patricia Henjewele.

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo amesema kuwa katika kutatua changamoto ya kupata soko la uhakika la bidhaa za ngozi, Wilaya hiyo imejipanga kuwatafutia maeneo wazalishaji wa ndani ambapo wote  watakaa sehemu moja kwa ajili ya uzalishaji na uuzaji  wa bidhaa hizo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maonesho ya bidhaa za ngozi yanayofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Mhe. Chongolo amesema kuwa mkakati huo utasaidia kuinua uhakika wa soko kwa wazalishaji.
Amefafanua kuwa maonesho hayo ya bidhaa za ngozi yanafanyika kwa mara ya kwanza katika Wilaya hiyo na kwamba ni lazima kila mwananchi ajenge utamaduni wa kupenda bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na kuwataka kuondokana na dhana ya kuona bidhaa zinazotoka nje ndio bora zaidi.
“Ukienda kwenye nchi za wenzetu hasa zilizoendelea, wao wanathamini kwanza cha kwao, cha mwingine badae, nasisi tukifikia hatua hiyo tutafanikiwa sana, lakini tutafikaje hapo ni la zima kuanzia sasa tuamke tuanze kupenda vya kwetu,” amesema Mhe. Chongolo.
Mhe. Chongolo ameongeza kuwa uwepo wa maonesho hayo utaongeza tija na mipango madhubuti ya kuhakikisha kuwa mpango huo unakuwa endelevu sambamba na kuongeza wigo mpana wa kutangaza bidhaa hizo na wananchi kupenda kuzitumia.
“Uwepo wenu hapa utawezesha wale wananchi ambao wanakuja kununua bidhaa zenu, ndio watakuwa mawakala kwa wananchi wengine ambapo na wao watapenda kuja kununua bidhaa hizi bora na nzuri za kitanzania,” ameongeza.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kawe, Mhe. Muta Rwakatare amempongeza Mhe. Chongolo kwa kubuni na kufanikisha kuwepo kwa maonesho hayo.
Ameongeza kuwa kutokana na umahiri aliokuwa nao mkuu huyo wa Wilaya wa kutatua changamoto mbalimbali za wananchi, anaamini kuwa sasa ni wakati wa wajasiriamali hao kunufaika kwani changamoto zao pia zimefikia kikomo.
Ameongeza kuwa Rais Dk. John Magufuli amekuwa mstari wa mbele kusisitiza uchumi wa viwanda na kwamba hadi sasa tayari adhma hiyo imefanikiwa kwa asilimia kubwa.
Naye Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Dk. Patricia  Henjewele amesema kuwa wazo la kuwepo kwa maonesho hayo lilitolewa na Mhe. Chongolo wakati wa maonesho ya nanenane ambapo alihitaji kuandaliwa kwa mpango kazi wa kuwa na maonesho hayo.
Amesema kuwa kabla ya kufanyika kwa maonesho hayo, awali yalifanyika mafunzo ya siku nne ambayo yaliendana sambamba na maonesho ya bidhaa hizo kwa siku moja yaliyofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
 Dk. Henjewele amesema kuwa maonesho hayo ya siku nne yatafikia kilele Disemba 15 ambapo bidhaa zote za ngozi ikiwemo viatu, mikoba, mikanda na mabegi ya shule ya wanafunzi yanapatikana hapo.

No comments:

Post a Comment