WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, ameiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuendelea kutekeleza mkakati wake wa ufadhili wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo ya barabara.
Ameyasema hayo jijini Dodoma, wakati Waziri huyo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo kuhusiana na maendeleo na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara inayofadhiliwa na benki hiyo.
“Tunawashukuru AfDB kwakuwa miongoni mwa wadau muhimu katika kutoa ufadhili wa utekelezaji na uboreshaji wa barabara nyingi nchini, tunaomba muendelee na ufadhili kwani bado tunahitaji kuendelea kuunganisha mtandao wa barabara kati yetu na nchi jirani”, amesema Waziri Kamwelwe.
Aidha, Waziri huyo amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka 11 iliyopita Benki hiyo imetoa kiasi cha fedha zaidi ya shilingi Trilioni mbili (2) kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara zenye jumla ya urefu wa kilometa 1,655 ambapo kati ya hizo kilometa 1,168 zimeshakamilika na kilometa 487 bado zinaendelea na ujenzi wake.
Ametaja baadhi ya miradi ya barabara iliyofadhiliwa na Benki hiyo na ambayo imekamilika kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo ni ukarabati wa barabara ya Arusha - Namanga (km 105), barabara ya Singida - Babati - Minjingu ( km 223.5), barabara ya Iringa - Dodoma (km 260) na barabara ya Namtumbo - Tunduru (km 193).
Ameongeza kuwa miradi mingine ya barabara inayoendelea kutekelezwa kupitia ufadhili wa Benki hiyo kuwa ni ujenzi wa barabara ya Tabora – Koga - Mpanda (km 349), barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka kwa Awamu ya II, barabara ya Tanga – Pangani - Bagamoyo (km 246), barabara za mzunguko katika jiji la Dodoma, na ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Msalato jijini Dodoma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB, Amos Cheptoo, amesema kuwa AfDB itaendelea kuunga mkono na kufadhili miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara lengo ni kuifanya Afrika kuendelea kiuchumi.
Amesema kuwa lengo la kuja kwake Tanzania ni kuangalia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki hiyo ili kuona maendeleo yake.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment