WAZIRI wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa,Paramagamba Kabudi amezitaka nchi za jumuiya ya Afrika mashariki kuwekeza katika sekta ya miundo mbinu ili kuwa na nishati ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. Alisema hatua hiyo itawezesha biashara kukua kwa nchi za jumuiya hiyo kiwemo kuongeza sayansi ,Teknolojia na ubunifu kwa Vijana wenye ujuzi wa kufanyakazi kwenye viwanda hivyo.
Ameyasema hayo katika mkutano wa Wafanyabiashara zaidi ya 1000 wa nchi za Afrika mashariki ulioandaliwa na Baraza la Wafanyabiashara wa nchi za Afrika Mashariki (EABC) unaofanyika kwa siku mbili jijini Arusha na kwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya jumuiya ya Afrika Mashariki.
Prof.Kabudi amesema kuwa,nchi zilizo nyuma katika maendeleo ya viwanda zinapaswa kusaidiwa ili kupata viwanda na kuweza kuzalisha bidhaa na kuuza kwenye soko la pamoja la jumuiya ya Afrika Mashariki.
"lazima nchi ziwe na viwanda vya kutosha na kufanyabiashara nzuri, kwa sababu jumuiya ni ya watu wote na lazima iwanufaishe wananchi wote," Amesema.
Naye waziri wa viwanda na biashara Innocent Bashungwa amesema kuwa uchumi wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki lazima ujengwe kupitia sekta binafsi za viwanda, kilimo, Mifugo na kuimarisha miundo mbinu.
Amesema serikali ya Tanzania inajitahidi kuweka mazingira Bora kwa wafanyabiashara ili biashara zao zinakua na kuhakikisha wanafanyabiashara nje ya Tanzania bila kikwazo chochote. Waziri Bashingwa ametumia wasaa huo kuwakaribisha wawekezaji kuja hapa nchini kuwekeza viwanda kwa ajili ya vifungashio na kuviuza katika nchi wanachama.
Baadhi ya Wafanyabiashara waliohudhuria mkutano huo, Lomayan Laizer na Jiten Shah Mwanzilishi wa kampuni ya Quickmarc wamepongeza mazingira mazuri yanayotolewa kwenye nchi za ukanda huu na kuwataka kuangalia kwa kina na kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo ushuru na tozo mbalimbali.
Walisema kuwa pia vikwazo katika mipaka wakati wanaposafirisha bidhaa zao kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine imekuwa ni shemu ya changamoto hususani vipimo vya ubora na kuwataka wakuu wa jumuiya hiyo kuboresha na uwezekano wa kuondoa vikwazo hivyo ili kuwarahisishia Wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa urahisi zaidi.
Naye Erhard Mlyansi ambaye ni Afisa masoko mkuu wa kampuni ya Motisun Group kutoka jijini Dar es Saalamu inayotengeneza bidhaa mbalimbali za ujenzi na juisi ya Sayona amelalamikia hatua ya kuigwa kwa bidhaa zao na kuuzwa katika nchi za jumuiya ya Afrika mashariki Jambo ambalo limekuwa likiwasababishia usumbufu kibiashara.
No comments:
Post a Comment