TANZANIA YA KWANZA KUTOA MAFUNZO YA KUTUMIA AFYA MOJA KUTATHIMINI HATARI YA VIMELEA HATARISHI VYA MAGONJWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 23 November 2019

TANZANIA YA KWANZA KUTOA MAFUNZO YA KUTUMIA AFYA MOJA KUTATHIMINI HATARI YA VIMELEA HATARISHI VYA MAGONJWA

Mwezeshaji wa   Kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Benezeth Lutege akifafanua namna ya kufanya Tathmini  ya vimelea hatarishi vya magonjwa kwa kutumia Dhana ya Afya moja wakati  wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta za afya na wadau wa Afya moja kutoka  ngazi za Halmashauri mkoani Arusha, tarehe 22 Novemba , 2019.

KWA mara ya kwanza Barani Afrika, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kufanya mafunzo katika ngazi ya mkoa na Halmashauri kwa kutumia dhana ya Afya moja  kuwajengea uwezo wadau wa Afya moja juu ya namna ya  kufanya tathmini ya vimelea hatarishi vya magonjwa. Mafunzo hayo yamewakutanisha wadau wa Afya moja na wataalam kutoka sekta za afya ya binadamu, wanyama pori, mifugo, kilimo na mazingira. Wadau hao na wataalam kutoka sekta hizo za afya wamepata mafunzo ya namna ya kufanya tathmini hiyo kwa magonjwa ya Kichaa cha mbwa, Kimeta na Ugonjwa wa Brusela (Ugonjwa wa Kutupa mimba kwa wanyama).

Kufuatia nchi ya Tanzania kuwa imepiga hatua katika uratibu wa  masuala  ya Afya moja, ambayo ni dhana inayojumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo, kilimo na  mazingira katika kujiandaa, kufuatilia  na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu. Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Dawati la Uratibu wa Afya moja kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa  (FAO) imeratibu mafunzo hayo  yaliyotolewa na wakufunzi wa hapa nchini waliojengewa uwezo  na wataalamu kutoka Makao makuu ya  Shirika la Afya Duniani (WHO), Makao makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa  (FAO), pamoja na Shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (OIE).

Akiongea wakati wa kufunga mafunzo hayo tarehe 22 Novemba 2019,Jijini Arusha, Mkurugenzi wa Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, amebainisha kuwa ushirikiano wa wadau wa Afya moja na wataalam na sekta za Afya  kwa kutumia dhana ya Afya Moja hivi sasa ni agenda ya dunia nzima. Aidha amefafanua kuwa  dhana hiyo inapunguza gharama katika kushughulikia tishio la magonjwa  yanayotokana na vimelea vyenye uwezo wa kutoka kwa wanyama na kwenda kwa binadamu na hata mimea (mazingira) na kusababisha magonjwa na hata usugu wa vimelea vya magonjwa.

“Wadau wa afya moja wanawajibika kupanga mikakati mbalimbali ya udhibiti, ulinzi na usalama katika kuzuia, kujiandaa na kukabali magonjwa ambukizi. Moja ya mkakati ulioibuliwa Kitaifa na kimataifa ni kujiandaa kwa kuwafundisha  wataalam wa sekta mbalimbali za  afya jinsi ya kufanya tathmini ya  hatari ya vimelea vya magonjwa ambukizi kwa ushirikiano.” Amesema . Kanali Matamwe.

Kwa upande wake, Mwezeshaji wa Mafunzo hayo kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa  (FAO), Tanzania, Bi. Niwael Mtui amefafanua kuwa Shirika hilo moja ya kipaumbele chake ni kupunguza umasikini na kuongeza kipato cha wananchi, hivyo Shirika hilo linashirikiana na serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, katika kujenga uwezo wa  ndani ya nchi kwa kuwafundisha wataalam wa sekta za Afya katika kudhibiti magonjwa ambapo uwezo huo utasaidia kuimarisha afya ya binadamu na mifugo na hatimaye kipato kitaongezeka na umasikini utapungua

Wakiongea kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo  hayo wamebainisha kuwa  wamekuwa wakifanya tathmini za vimelela hatarishi vya magonjwa hapa nchini lakini tathmini hizo zimekuwa ni za kisekta kwani hazikuwa zinazingatia ushirikiano kwa maana ya dhana ya Afya moja. Aidha walifafanua kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutumia Dhana ya Afya moja kwa kuwa inapunguza gharama katika kushughulikia tishio la magonjwa  yanayotokana na vimelea vyenye uwezo wa kutoka kwa wanyama na kwenda kwa binadamu na hata mimea (mazingira) na kusababisha magonjwa na hata usugu wa vimelea vya magonjwa.

Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughuli za Afya moja nchini. Kwa kutambua umuhimu huo  Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati la Uratibu wa Afya moja  kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa  (FAO) na wadau waliandaa na kuratibu mafuzo hayo, ambapo wataalamu wa sekta za Afya na Wadau wa Afya moja kutoka Halmashauri nne za mkoa wa Arusha (Halmasahauri ya Arusha, Monduli, Ngorongoro na Karatu) walishirki mafunzo hayo.

No comments:

Post a Comment