Na Eleuteri Mangi, Dodoma
MICHEZO ni nyenzo madhubuti katika kulinda afya za wanadamu kwa kuwajengea uimara na ustahimilivu, kukuza stadi za kijamii kiubunifu na kiuongozi ili kuwawezesha wanamichezo na watu wote kujifunza vitu vipya vinavyoweza kuchangia kutunza afya zao ili waweze kujiletea maendeleo yao wenyewe na taifa kwa ujumla.
Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 inatambua umuhimu wa michezo ikiwemo kuhamasisha Umma wa Watanzania kushiriki katika michezo na mazoezi ya viungo. Kwa kutambua jambo hilo, Serikali imewezesha upatikanaji wa viwanja na vifaa vya michezo vilivyo bora na vya kutosha kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya michezo nchini.
Kama taifa, kumekuwa na mtazamo chanya kwa viongozi kuthamini michezo kuanzia ngazi ya Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa kupitia mikoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji, mitaa na vitongoji.
Kwa kulitambua na kulithamini suala la michezo kwa watu wa rika zote kuwa ni muhimu kwa afya, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan mwaka 2016 alipokuwa akizindua kampeni ya kitaifa ya kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwenye viwanja wa Leaders Club jijini Dar es Salaam aliagiza watu katika maeneo yao nchini kushiriki kufanya mazoezi ambayo ni sehemu ya michezo.
Ili utaratibu wa kufanya mazoezi uwe endelevu, Makamu wa Rais alisisitiza “……….kila Jumamosi ya pili ya mwezi itakuwa siku ya mazoezi kwa afya, kwa sababu mazoezi ni afya na nawaasa wananchi kufanya mazoezi na kuanzisha na kujiunga na vikundi vya mazoezi na Serikali itatimiza wajibu wake wa kuweka mazingira mazuri ya kufanyia mazoezi kote nchini.”
Wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa katika kulifanyia kazi agizo hilo kwa kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi ambao umeongeza idadi ya vikundi vya mazoezi ya pamoja katika maeneo mbalimbali ya nchini.
Hamasa ya kufanya mazoezi sasa imekuwa nzuri ambapo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zimeanzisha utaratibu wa kuwa na bonanza, matamasha ya michezo pamoja na vilabu vya kufanya mazoezi. Hatua hii imekuwa ni chachu mpya ya kutekeleza agizo la Makamu wa Rais Mama Samia la kufanya mazoezi kwa manufaa ya afya za Watanzania.
Akiwasilisha Bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2019/2020 ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo Dkt. Harrison Mwakyembe aliliambia bunge na Watanzania wote kuwa, miongoni mwa majukumu ya sekta ya michezo ni kuratibu na kusimamia maendeleo ya michezo nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika michezo.
Mojawapo ya vitu vinavyoshirikisha watu wengi kujiunga na kufanya mazoezi ni kuwa na matamasha ya michezo mbalimbali ambayo yanalenga kuhamasisha wananchi kushiriki katika michezo ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya viungo ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi hapa nchini.
Magonjwa hayo hutokana na mitindo isiyofaa ya maisha kama matumizi ya tumbaku, lishe duni, matumizi ya pombe kupita kiasi, pamoja na kutoshughulisha mwili au kutofanya mazoezi ya viungo mara kwa mara. Magonjwa kama kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na mishipa, saratani, pumu na magonjwa ya akilini miongoni mwa magonjwa hayo, ambapo yasipodhibitiwa huwa na sugu na yenye kuhitaji gharama kubwa kuyatibu.
Hapo awali, magonjwa hayo yalikuwa yakiwaathiri watu wenye umri mkubwa zaidi ya miaka 45, lakini kwa sasa yanazidi kuathiri watu watu wengi wakiwemo watoto wenye umri mdogo.
Naibu Wiziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza hivi karibuni akiwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa tamasha la michezo la wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza lililofanyika Novemba 09, 2019 katika uwanja wa Jamhuri Dodoma alihimiza watu kuchukua uamuzi wa kufanya mazoezi ili kujenga afya zao.
“Mazoezi ni jambo lolote linalohusisha misuli na kusababisha kuongezeka kwa mapigo ya moyo na kasi ya kupumua. Wataalam wa afya wanasema kuwa kiwango cha mazoezi kinacholeta faida ni mazoezi yasiyopungua dakika 30 kwa siku angalau siku tatu kwa wiki na yanayomfanya mtu kutokwa na jasho” alisisitiza Naibu Waziri Shonza.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Shonza watumishi wanaofanya kazi ofisini wametakiwa kuongeza bidii ya kufanya mazoezi kulingana na mtindo wa maisha ya mtumishi mmoja mmoja kuendana na hali yake ya maisha.
Kwa watumishi wa umma na sekta binafsi pamoja na watu wengine wanaotumia magari, wanapaswa kupanga shughuli ambazo zitawafanya kila siku watembee kwa miguu, wanaoishi au kufanya kazi ghorofani wajitahidi na wajizoeshe kutumia ngazi kila siku badala ya lifti, mtu anapokwenda mahali popote watumie njia ndefu kutembea badala ya njia ya mkato pamoja na kupunguza muda wa kutazama televisheni, badala yake muda huo utumike kufanya shughuli zinazotumia viungo vya mwili kama kufua, kuosha vyombo, kuosha gari, kusafisha nyumba, kazi za bustani na kufyeka majani ambazo zinasaidia kujenga utimamu wa mwili.
Naibu Waziri Shonza ametoa rai kwa waajiri kuboresha mazingira ya kazi kwa kuhakikisha watumishi wao wanashiriki katika michezo na kufanya mazoezi hata maeneo yao ya kazi na kutoa mfano wa kuanzisha timu mbalimbali za michezo na kutenga siku maalum katika mwezi kwa ajili ya mabonanza ya michezo. Mazingira rafiki ya kufanyia mazoezi kazini ni pamoja kutenga vyumba vya mazoezi na na kununua vifaa vya michezo. Hatua hiyo itaimarisha afya za watumishi na kupunguza gharama za matibabu katika taasisi husika.
Aliongeza kuwa ili kufanya mazoezi kuwa endelevu, maafisa michezo na utamaduni wa mikoa na wilaya wana wajibu wa kuongeza uhamasishaji na uundaji wa vikundi vya mazoezi ya pamoja katika maeneo yao.
Wizara nyingine zenye uhusisano na mchango katika kufananikisha wananchi kufanya mazoezi ni Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Wizara hizo zina mamlaka ya kusimamia na kuweka mazingira bora ya watu kufanya mazoezi kwa kuendelea kutenga viwanja vya michezo na kuzuia uuzaji wa maeneo ya wazi hususani viwanja vya michezo na kuboresha barabara za waenda kwa miguu na baiskeli ili kuhamasisha watu kutembea na kuongeza usalama wa mazoezi.
Aidha, mamlaka za usafiri, zinawajibu wa kuboresha usafiri wa jumuiya ili kuongeza idadi ya watu wanaotumia usafiri wa jumuiya kwa sababu tafiti nyingi zinaonesha kuwa utumiaji wa usafiri wa jumuiya unaongeza uwezekano wa kutembea na kufanya mazoezi na hivyo kupunguza magonjwa yasiyoambukiza.
Matamasha ya michezo pamoja na matamasha mengine yakiwemo ya utamaduni yanatakiwa kuwa kichocheo cha kushirikisha vitu vingi ikiwemo michezo ya jadi na mashindano ya baiskeli katika maeneo mbalimbali ambayo yana mchango mkubwa katika kutunza afya za washiriki wa michezo hiyo.
Wakati wa matamasha hayo, ni vema wananchi wahamasishwe kupima afya zao hususani wa magonjwa yasiyoambukiza kwani tiba ya mapema ina manufaa kwa kuwa inapunguza uwezekano wa watu kupatwa na madhara zaidi. Hatua hiyo inaweza kuondoa magonjwa hayo moja kwa moja. Ili kuongeza hamasa ya wananchi na wanamichezo kupima afya zao, upimaji huo unapaswa kuwa ni wa bure ili watu wengi zaidi wapate fursa ya kupimwa.
Hivi karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa mwongozo wa kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambapo mataifa yameazimia kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu, (SDGs) ili kupunguza kwa theluthi moja vifo vya mapema vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ifikapo mwaka 2030.
Akizungumzia mwongozo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tedros Adhanon Ghebreyesus alisema, “Zaidi ya nusu ya watu duniani wanaishi mijini, na idadi yao inaongezeka. Viongozi wa miji wanapaswa kuchukua maamuzi ambayo yataboresha afya za wakazi wao, ili miji iweze kuchipua na kustawi. Kila mtu anapaswa kupata huduma ambazo zitaboresha afya, huduma za usafiri wa umma ziwe salama, makazi ya nje yawe safi na salama, mlo uwezo mzuri na huduma za afya ziwe bora.”
Naye Balozi wa WHO katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) na majeraha, Michael Bloomberg alisema kuwa shirika hilo lipo mstari wa mbele katika kusambaza mikakati hiyo duniani kote ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watu.
“Tunafanya kazi kuhamasisha uelewa miongoni mwa viongozi wa miji na watunga sera kuhusu manufaa halisi yanayoweza kupatikana pindi programu hii ya kuboresha miji inapofanya kazi.” alisisitiza Balozi Bloomberg.
Ni kweli, wataalamu wa afya wanashauri kuwa ni vema kila mtu awajibike kuitunza afya yake kwa kufuata mtindo bora wa maisha kwani afya njema ni msingi wa maendeleo. Hatua hii inaunga mkono kauli mbiu tamasha la michezo la wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ambukiza inayosema “Tutembee pamoja katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.”
No comments:
Post a Comment