BENKI ya NMB imetoa msaada wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 30 kusaidia ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wilayani Chato, Mkoa wa Geita. Vifaa vilivyo kabidhiwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo, ni pamoja na mifuko 500 ya simenti na matofali 13,335 huku ikiahidi kuendelea kuchangia zaidi ujenzi wa kiwanja hicho hapo baadae.
Akikabidhi msaada huo katika hafla fupi, Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Bw. Abraham Augustino alisema NMB itaendelea kusaidia kukuza michezo kwani inatambua inaumuhimu mkubwa katika kulinda afya ya mwili hasa kwa vijana.
"Huu ni utaratibu ambao NMB imejiwekea katika kusaidia jamii nyanja mbalimbali kwa mwaka huu. Hadi sasa tumetumia takribani shilingi milioni 900 nchi nzima kusaidia shughuli anuai za kijamii," alisema Bw. Augustino.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho pamoja na Mkurugenzi wake, Eliud Mwaiteleke wakipokea msaada huo waliishukuru na kuipongeza Benki ya NMB kuchangia na kuinua michezo katika wilaya hiyo.
Kabeho alisema ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wilayani Chato ni miongoni mwa mpango mkakati wa kuhakikisha wilaya inasonga katika maendeleo kimichezo.
Naye, Mwaiteleke akizungumza katika hafla hiyo aliongeza kuwa uwanja huo utakaokuwa na uwezo wa kuchukua watu 3000 kwa pamoja utasaidia michezo na wanamini utaweza kuvichagiza vilabu vikubwa vya ligi kuu kama Simba SC, Yanga Africa na Azam FC kutumia katika shughuli za kimichezo.
"Tunatarajia baada ya kukamilisha uwanja huu utavivutia vilabu vikubwa kama Simba na Yanga kuutumia hata kuweka kambi zao katika maandalizi ya mashindano mbalimbali. Tunaomba wafadhili wengine wajitokeze kuunga mkono NMB ili kufanikisha ujenzi wa uwanja wetu," alisema.
No comments:
Post a Comment