Na Teresia Mhagama - Geita
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga ameeleza kuwa wakandarasi wa umeme
vijijini wanaosuasua katika utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini
wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza (REA III) hawatapewa kazi katika miradi
inayofuata.
Aliyasema hayo wilayani Mbogwe, Mkoa wa
Geita mara baada ya ya Bodi ya REA ikiongozwa na Mwenyekiti
wake Wakili Julius Kalolo kufanya ziara ya kukagua kazi ya
usambazaji umeme vijijini wilayani Bukombe na Mbogwe.
" Tuko katika ziara hizi si kutoa
maelekezo tu bali pia tunafanya tathmini za wakandarasi kwani tutakuwa na
kanzidata itakayoonesha wakandarasi wanaotekeleza miradi kwa wakati na
viwango vinavyotakiwa na wale wanaosumbua katika utekelezaji wa mradi
unaoendelea." Alisema Mhandisi Maganga.
Aliongeza kuwa, kanzidata hiyo itasaidia
kuwatambua wakandarasi wote wasiofaa kupewa tena nafasi ya kutekeleza miradi ya
umeme vijijini inayofuata hivyo aliwataka wakandarasi hao wajipange
kufanya kazi vizuri.
Aidha, aliwataka wakandarasi wote
kuzingatia agizo la Serikali la kuhakikisha kuwa ifikapo Disemba 31 mwaka
huu, vijiji vyote vilivyo katika mradi wa REA III, mzunguko wa
kwanza vinapelekewa umeme.
Kuhusu mkandarasi anayesambaza umeme mkoani
Geita, kampuni ya Whitecity Guangdong JV, alimuagiza kuwa ifikapo tarehe 31
Disemba awe amepeleka umeme kwenye vijiji alivyopangiwa na kuwasilisha mpango
kazi utakaoonesha pia kazi alizopanga kufanya katika kila Wiki.
Bodi ya REA kwa upande wake, ilimuagiza
mkandarasi huyo kutekeleza ratiba za upelekaji umeme katika maeneo yote ambayo
Bodi hiyo imetembelea mkoani Simiyu na Geita na kumweleza kuwa haitaacha
kufuatilia utekelezaji wa ahadi hizo ili wananchi wapate nishati ya umeme.
Aidha, Bodi hiyo ilimuagiza mkandarasi
kuhamasisha matumizi ya vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) ili kuwaondolea wananchi
gharama kufanya wiring ndani ya nyumba na kwamba kipaumbele kiwe ni
wajane, wazee na walemavu.
Pia Bodi hiyo iliwaasa viongozi wa vijiji
katika maeneo mbalimbali nchini ambapo miradi ya umeme vijijini inaendelea
kutekelezwa, kuwahamasisha wananchi ili waunganishiwe na huduma ya umeme hivyo
miradi hiyo kuwa na tija.
Bodi hiyo pia ilikagua kazi ya usambazaji
umeme wilayani Nyang'hwale mkoani Geita ambapo mkandarasi alieleza kuwa ndani
ya Wiki hii atawasha umeme katika Vijiji Saba.
No comments:
Post a Comment