Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Shein. |
Na Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Shein ameutaka uongozi wa Wizara ya Afya kuwa na mpango maalum wa ajira kwa wafanyakazi wa Afya katika kipindi cha mwaka mzima, kutegemea na upatikanaji wa fedha kutoka Serikalini.
Dk. Shein amesema hayo Ikulu Mjini Zanzibar, wakati akipokea taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2018/19.
Alisema ili kufanikisha jambo hilo ni vyema yakawepo mashirikiano ya karibu kati ya Wizara hiyo na Wizara ya Fedha ili kuwa na mpangilio mzuri wa ajira utakaowawezesha wanafunzi wanaomaliza masomo ngazi za shahada katika nyanja tofauti kuajiriwa kulingana na mahitaji yaliopo.
Alisema kuwepo kwa utaratibu huo utawawezesha wanafunzi wa fani mbali mbali za afya wanaosoma nje ya nchi, akitolea mfano wa Cuba kuwepo kwenye mpango huo na kuajiriwa mara tu baada ya kumaliza masomo yao.
“Ni muhimu kuwa na mpango kuliko kufanyakazi kwa kushtukiza”, alisema.
Aidha, aliutaka uongozi huo kuongeza nguvu katika utoaji wa mafunzo ili kuwawezesha wataalamu waliopo kuwa na uweo zaidi katika kukabiliana na magonjwa mbali mbali.
Alisema kuna umuhimu kwa Viongozi wa Wizara hiyo kukaa pamoja na Mshauri wa Rais wa masuala ya Afya, ili kuona utaratibu bora utakaokubalika kwa wafanyakazi, madaktari na madaktari bingwa wa kufanya kazi katika muda wa ziada na kubainisha umuhimu wa wafanyakazi hao kupata stahiki zao kwa mujibu wa sheria.
“Serikali haikatai kulipa wafanyakazi, lakini uadilifu uwepo kati ya wafanyakazi na Serikali”, alisema.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliutaka uongozi huo kujipanga vyema katika uendeshaji wa Hospitali ya Mnazimmoja, kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa katika hospitali hiyo, hatua inayotoka na matarajio makubwa waliyonayo.
Alisema changamoto hiyo inafanana na ile ya wagonjwa wengi kuhitaji matibabu nje ya nchi, hususan nchini India.
Alisema Serikali imedhamiria kupunguza wimbi la wagonjwa kukimbilia nje ya nchi kwa kuimarisha uwepo wa vifaa bora vya tiba, akibainisha azma ya Serikali ya kununua mashine ya kisasa ya Citscan,ili kuendana na mahitaji yaliopo.
Aidha, Dk. Shein aliipongeza Wizara hiyo kwa maandalizi bora ya taarifa ya utekelezaji, sambamba na kutekeleza vyema majukumu yao ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Nae, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, alisema kupitia Bajeti ya Wizara hiyo, Serikali imetenga fedha nyingi kwa lengo la kuimarisha huduma za afya ili kuleta ustawi bora na afya za wananchi.
Alisema utendaji na ufanisi wa Wizara hiyo unapimwa na wananchi kutokana na upatikanaji wa huduma bora kupitia katika hospitali zake na vituo vya Afya vilivyopo nchini.
Aliwataka watendaji kuimarisha usimamizi wa utoaji huduma, hususuan katika Hospitali ya Mnazi mmoja, ili kuondokana na malalamiko kutoka kwa wananchi.
Aidha, Katibu Mkuu wa Baraza La Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kujipanga na kuandaa utaratibu wa kuwapata wataalamu wapya katika maeneo tofauti, watakaoweza kuziba nafasi ya wataalamu waliopo baada ya kustaafu.
Alisema kuna haja ya uongozi huo kuhakikisha unakamilisha ahadi za Rais pamoja na yale yote yalioelekezwa katika Ilani ya CCM, kabla ya kufikia mwezi June, mwaka ujao.
Dk. Mzee, aliwataka viongozi hao kuongeza juhudi katika usimamizi wa majukumu yao, ili kufikia malengo yaliowekwa.
Nae, WazIri wa Wizara hiyo, Hamad Rashid Mohamed, alisema katika kipindi hicho Wizara imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa shughuli zake, ikiwemo kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa kwa wastani wa asilimia 91 katika mwaka wa 2018/19.
Alisema mafanikio hayo ni makubwa ikilinganishwa na asilimia 83 katika mwaka wa 2017/2018, pamoja na asilimia 50 katika mwaka wa 2016/2017.
Alisema sambamba na hilo kulikuwa na ongezeko la watendaji 662 wa fani za Afya wakiwemo madaktari 55 na wauguzi 114.
Aidha, alisema kulikuwa na uimarikaji wa huduma za vipimo pamoja na upatikanaji wa huduma za matibabu.
Waziri Hamad, alisema Wizara ilifanikiwa kuzipandisha daraja Hospitali za kijiji za Makunduchi na Kivunge na kuwa Hospitali za Wilaya, hatua aliyobainisha kuwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kifungu cha 102(c)).
Vile vile alisema mafanikio mengine yaliopatikana ni kukamilika kwa jengo jipya la Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na kupatikana kwa mashine ya uchunguzi wa Vinasaba (DNA), sambamba na kukamilika kwa Vituo 19, vilivyobainishwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015 kifungu cha 102(d).
Pia, alisema Wizara imeanza matayarisho ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa na kufundishia katika eneo la Binguni, Wilaya Kati Unguja, ambapo michoro na makisio ya gharama (BOQ) tayari yamekamilika.
Katika hatua nyengine, Waziri huyo alisema katika utekelezaji wa shughuli hizo, Wizara ilikabiliana na changamoto mbali mbali, ikiwemo upungufu wa wafanyakazi katiika baadhi ya maeneo ya utoaji huduma, hususan madaktari bingwa. wataalamu wa lishe, wataalamu wa usingizi na epidemiologia.
Aidha, alisema kulikuwa na ongezeko la wagonjwa wanaohitaji kupatiwa huduma za afya hususan katika Hospitali ya Mnazimmoja.
Sambamba na hilo, alibainisha kuwa pia kulikuwa na changamoto ya ongezeko la wagonjwa wanaohitaji kupatiwa huduma za Afya nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment