NDANI YA MIAKA 10, NYERERE ALITUVUSHA KWENYE MITIHANI MIGUMU MITANO... - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 14 October 2019

NDANI YA MIAKA 10, NYERERE ALITUVUSHA KWENYE MITIHANI MIGUMU MITANO...

Hayati Mwalimu Julius Nyerere, baba wa taifa la Tanzania.

Tulikotoka: 

Ndani Ya Miaka Kumi, Nyerere Alituvusha Kwenye Mitihani Migumu Mitano...

Ndugu zangu,

HISTORIA ni Mwalimu Mzuri. Na tuamini, kuwa ili mwanadamu ajue mahali alipo na anakokwenda, ni muhumu awe na uelewa na alikotoka. Aijue historia yake ili imsaidie kwenye kujitambua.

Zamani sana nilipata kuyaandika haya kufuatia mada niliyoianzisha juu ya hamu inayojengeka kwenye jamii ya kutamani udikteta bila kujua udikteta maana yake nini.

Nilimjibu mmoja wa wachangia mada ndugu Galinoma kama ifuatavyo;

"Galinoma, foleni za unga haikumaanisha udikteta. Dunia ilikuwa tofauti na sasa. Dunia ilikuwa kwenye vita baridi na mapambano ya kiitikadi; Ujamaa dhidi ya Ubepari. Mimi ni Mjamaa, na zaidi ni Social Democrat.

Nimekulia katikati ya mapambano hayo ya kiitikadi. Nchi yetu wakati huo ilipitia mitihani migumu mitano kama taifa;

Mtihani wa kwanza; migogoro miwili ya mafuta duniani.

Ni kati ya 70 na 73. Mtihani wa kwanza wa mafuta ni mwaka 1970. Wa pili mwaka 1973.

Mtihani wa tatu ni ukame wa mwaka 74. Watanzania tulikula 'Unga wa Yanga' kwa maana ya unga wa njano wa msaada kutoka Marekani.

Mtihani wa nne ni kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977. Kama nchi tukajikuta tunaanza upya. Hatuna hata ndege moja na wala vichwa  vya treni. Wakenya walitufanyia uhuni ( Walivunja Jumuiya wakati ndege za jumuiya ziko Embakasi na vichwa vya treni viko Kisumu). Leo tuna ndege zetu za maana 8 na SGR tunajenga.

Mtihani wa tano ni Vita vya Kagera 1978-79.

Ndani ya miaka kumi nchi yetu ilipitia mitihani migumu mitano.

Nilikuwa na miaka kumi na moja pale Kinondoni Biafra, nilipomsikia kupitia redio, Julius Nyerere akitangaza vita dhidi ya dikteta Idd Amin. Ni Idd Amin aliyetuvamia na kuchukua sehemu ya ardhi yetu.

Usiku ule niliyaona magari ya kijeshi yakipita nje ya nyumba yetu, pale Morocco rd Kinondoni Biafra.

Umeme ulikatwa, magari yale yalikuwa yakitokea kambi ya Lugalo kwenda mpakani.

Nikiwa bado mtoto mwaka ule wa 1979 vita vilipomalizika. Nilikuwepo pia na watoto wenzangu pale uwanja wa taifa siku ya kuwapokea rasmi mashujaa wetu na kutangazwa kumalizika kwa vita.

Mbali ya kumpoteza rubani wetu kwenye ndege ya kivita iliyokuwa ituangukie uwanjani, lakini rubani akajitahidi aende akaanguke nayo nje ya uwanja.

Nakumbuka Julius Nyerere alibaki amekaa akiwa amekunja miguu na kushika tama. Alionekana kutulia.

Na ilipofika muda wa kuhutubia, Julius alitoa hotuba muhimu yenye kutuandama hadi leo.

Aliamua kuacha kuzungumzia ajali ile, bali, alirudia kusema kuwa vita si lelemama, na kwamba Watanzania tujiandae kufunga mikanda kwa miezi kumi na nane. Kimsingi alitangaza vita vingine vya kiuchumi.

Na hakika ikawa zaidi ya miaka 18, na hadi leo tuna makovu ya vita. Ni makovu ya majeraha ya kuumia kiuchumi.

Naam, ndani ya miaka kumi nchi yetu ilipitia mitihani mitano migumu.

Nyerere alijenga uongozi wa kitaifa uliojenga ushawishi na mshikamano wa kitaifa tukaweza, hata kwa tabu, kuvuka mitihani hiyo mitano na tukabaki salama, kama Taifa.

Daima Atakumbukwa.

Na Maggid Mjengwa.

No comments:

Post a Comment